HABARI MPYA LEO  

VIJANA WATANO WANYONGWA KIKATILI JIJINI ARUSHA

By Maganga Media - Apr 23, 2012

Habari za kusikitisha kutoka Jijini Arusha  zinaeleza kuwa jumla miili ya watu watano imepatikana mapema alfajiri katika Mto Nduruma uliopo maeneo ya Tengeru, baada ya kunyongwa na watu wasiojulikana hadi kufa. Miili hiyo ya marehemu hao vijana, imekutwa na majeraha kichwani na alama za minyororo shingoni na wengine kamba za katani kama inavyoonekana pichani

WATU wanne wanaosadikiwa kuwa ni madereva wa pikipiki maarufu bodaboda ambao waliuawa kwa kunyongwa kisha kuvunjwa shingo na watu wasiotambulika usiku wa kuamkia juzi wilayani Arumeru mkoani Arusha, inadaiwa kuwa ni wezi waliokuwa wakisumbua katika Kata ya Sombetini ndani ya Jiji la Arusha.

Kuuawa kwa watu hao kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye na maiti zao ziko katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

Habari kutoka kwa wakazi wa Sombetini zilidai kuwa mpango mkali uliandaliwa kuwasaka wezi hao ambao hufanya kazi ya kuendesha bodaboda kama kisingizio, lakini ikifika saa 6 hadi 8 usiku, hufanya kazi ya kuvunja nyumba Sombetini na Nguselo.

Mmoja wa watoa habari aliyekataa kutajwa jina gazetini, alidai kuwa mpango huo ulisukwa
kimyakimya kwa kuhusisha watu wachache wa Sombetini, wa kuwasaka kila walipokuwa wakifanya kazi yao ya bodaboda.

Vyanzo vingine vilieleza kuwa bado kuna mwizi mmoja ambaye ni kiongozi wa waliouawa, anatafutwa na watu hao wa Sombetini ili apate kile walichopata wenzake kwani ndiye mfadhili mkubwa wa ujambazi.

Maiti hizo zilikutwa zikiwa na kamba za katani shingoni, mikononi na minyororo shingoni na mikononi ambayo inasadikiwa kutumika kuwafunga watu hao kabla ya kuwanyonga, hali inayoonesha kuwa kulikuwa na purukushani kabla ya kunyongwa kwao.

Baadhi ya watu waliofika kutambua miili hiyo, waliitambua mitatu kati ya minne ambayo ni Jumbe Saitobi, Elly Lotti, Boshu Maombi; wote ni wakazi wa Arusha na wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35.
 

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII