HABARI MPYA LEO  

WALIOCHAGULIWA KIDATO CHA TANO 2012

By Maganga Media - Mar 27, 2012


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, huku idadi yao ikishuka kwa asilimia 13.34 ikilinganishwa na mwaka jana. Akitangaza majina hayo Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema kutokana na hatua hiyo, shule nyingi hasa zinazochukua wanafunzi wa mikondo ya sanaa na uchumi, zimekosa idadi ya wanafunzi kama ilivyotakiwa.

“Serikali ilikuwa imetenga nafasi 15,000 za wasichana, lakini waliopatikana ni 9,378 tu, nafasi zilizokuwa zimetengwa kwa wavulana ni 26,000, lakini waliopatikana ni 22,138,” alisema. Alisema wanafunzi 142 waliobakia, ufaulu wao haukuweza kutengeneza maunganisho yoyote ya masomo, kwa hiyo hawakupangwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

Mwaka 2010, wanafunzi 352,840 walifanya mtihani wa kidato cha nne, huku 40,388, sawa na asilimia 11.5 wakipata daraja la kwanza mpaka la tatu. Waliochaguliwa kuendelea na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa 36,366. Mulugo alisema mwaka 2011 wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 336,301, huku 33,577 sawa na asilimia 9.98 wakipata daraja la kwanza mpaka la tatu. Ufaulu huu umepunguza idadi ya waliochaguliwa kidato cha tano na vyuo vya ufundi kutoka wanafunzi 36,366 mwaka 2011 mpaka wanafunzi 31,516 mwaka 2012. Huu ni upungufu wa wanafunzi 4,850 sawa na asilimia 13.34,” alisema Mulugo.


Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII