Mada ya leo: UPOTEVU HUU WA VYETI MPAKA LINI?
By Mhariri - Aug 17, 2012
Katika pita pita zangu siku ya leo nikatokea Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA). Nilidhani kuwa shida yangu ni ndogo na labda nitaonekana mzembe sana kumbe matokeo yake yakawa tofauti kabisa. Ni kilio cha wengi, wakubwa kwa wadogo, jinsia zote. Baada ya kuwa nimehudumiwa na kuridhika na majibu ya afisa aliyekuwa kwenye kitengo hicho, nimeona nije kwenu wananchi tujadili kidogo juu ya suala hili.
Kama mada inavyosema ni upotevu wa vyeti. Nimekutana na foleni kubwa ya watu wenye tatizo la kupotelewa kwa vyeti vya kumaliza elimu ya sekondari kati ya kidato cha nne au kidato cha sita kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuibiwa au kudondosha bila kujijua.
Katika gazeti la Habari leo la tarehe 17 August, 2012 ukurasa wa 30 ambao ni maalum kwa MICHEZO/MATANGAZO kati ya matangazo yote 14 yaliyopo hapo, matangazo 9 ni ya kupotelewa na vyeti vya kidato cha nne. Na kwa mujibu wa maelezo ya dada mmoja ambaye jina lake limefanikiwa kuonekana kwenye gazeti la leo anadai kuwa foleni ni ndefu mno. Alipoulizwa ilikuwaje hadi cheti chake kikapotea anasema alikuwa anatoka kupiga photocopy, na alipofika nyumbani akagundua kuwa tayari kimepotea. Alipofuatilia hajakipata, anaamini kilipotea. Hili ni janga.
Siwezi kumlaumu huyo aliyepoteza cheti kwa sababu yeyote ile, kwani hakuna anayependa hilo limtokee. Ninachotaka kujenga hoja ni juu ya madhara ya wimbi kubwa la kupotea kwa vyeti na athari zake kwa jamii yetu siku za usoni.
Utaratibu uliopo sasa, kama mtu amepoteza cheti chake cha elimu ya sekondari kinachotolewa na NECTA, anapaswa kufuata utaratibu wa kawaida wa kutoa ripoti kituo chochote cha polisi nchini, kisha kwenda kutoa tangazo la kupotelewa cheti katika magazeti ya serikali na kisha baada ya tangazo la gazetini kuchapishwa ataambatanisha hiyo taarifa ya upotevu wa cheti na nakala ya gazeti lenye tangazo lake ndipo taarifa zake za matokeo zitatumwa sehemu husika zinapotakiwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wewe uliyepoteza cheti hutapata nakala wala waraka wowote wa kuthibitisha matokeo yako wala kukutambulisha labda uendelee kutumia nakala ya cheti kama bado unayo na utakapotakiwa kutoa nakala halisi uende NECTA watatuma taarifa zako iwe kwa mwajiri au chuo kama unataka kuendelea na masomo.
Mpaka hapo, ninapata maswali manne (4) :
1. Ni kwa jinsi gani huyu mwanafunzi ataendelea kusumbuka na utaratibu huo wa kila akitaka uthibitisho asafiri kutoka huko aliko hata kama ni pembezoni mwa nchi hadi Dar es Salaam kuomba uthibitisho wake wa matokeo utumwe huko unapohitajika?
2. Ni waajiri wangapi katika kipindi hiki cha kugombania ajira ataweza kukuvumilia wewe uliyepoteza cheti utumiwe uthibitisho wa nakala yako wakati wapo watu wenye sifa kama za kwako na wana vyeti vyao halisi mkononi mwao? Endapo akikuajiri wakati anasubiria taarifa ya NECTA huoni kuwa ataundiwa tume kuwa amekula rushwa kwa kuwa umeajiriwa bila kuonesha cheti halisi?
3. 3. Kuna utaratibu gani wa kukibatilisha cheti cha awali kilichopotea na kuokotwa ambacho bila shaka kama hakijapatikana kitakuwa kinatumiwa na mtu mwingine mwenye nia mbaya? Ikiwa kwa mfano halisi kumekuwa na tabia ya mtu akipoteza simu au akiibiwa, wale walioiba simu hudiriki kuwatumia meseji watu walio kwenye orodha ya namba za simu ile kuwa, “mtumiaji wa simu hii amekufa, au kuwatapeli watu kwa kuwaomba pesa na mtumaji hutuma akiamini anamtumia mtu anayemfahamu kuwa mtumiaji wa namba ile kumbe siye.
Katika kupambana na hilo, unapotoa taarifa ya kuibiwa au kupotelewa namba yako ya simu wafanyakazi wa mtandao husika huifunga namba. Je kwa cheti kuna utaratibu wowote?
Nilishuhudia fomu ya kujaza kwa ajili ya kuomba vitambulisho vya raia wa Tanzania zoezi lililoendeshwa jijini Dar es Salaam. Katika fomu hiyo, kwa upande wa vitambulisho kuna sehemu ya kujaza namba ya vitambulisho kama ni leseni ya udereva, cheti cha kuzaliwa, cheti cha kumaliza elimu ya sekondari, kadi ya kupigia kura, na kadharika. Je, sehemu hiyo, kwa kuwa tayari imeshawekwa, haiwezi kuwa njia mojawapo nzuri ya kutumia ili kila mtu aorodheshe namba ya vyeti vyake hapo na pindi kitambulisho kikitoka, taasisi zinazohusika na ajira wataweza kufuatilia namba za vyeti na kama mtu atakuwa amepoteza cheti chake, kwa kutaja namba yake tu yatatokea matokeo yake kama ilivyo sasa katika utaratibu unaotumiwa na TCU katika kudahili wanafunzi wa elimu ya juu?
4. 4. Ni vyeti vingapi vimerudishwa kwa waliopotelewa baada ya kutangazwa? Je ni kweli kuwa wananchi hawavioni au kuviokota? Ni kwa nini jamii isijione kuhusika katika hili ili kuwasaidia wahusika?
Mwandishi wa makala hii hakuona umuhimu wa kuhoji upande wa pili kwa watendaji wa NECTA kwa kuwa ni hatua za awali tu hizi za kuangalia ukubwa wa tatizo na athari zake kwa jamii kupitia mjadala wa wazi, pindi taarifa ikiwa kamili utaratibu wa kuwasilisha maoni utafuatwa. Ni imani yangu kuwa NECTA wana sababu za msingi juu ya uamuzi wa kutotoa cheti wala maelezo ya matokeo kwa mtu aliyepoteza cheti isipokuwa kwa taasisi inayoyahitaji kupitia taarifa juu ya mtu husika, aliyepoteza atawasilisha maombi na matokeo yatatumwa moja kwa moja yanapotakiwa kwa gharama za muombaji.
Miongoni mwa madhara ambayo Maganga Media inaziona ni pamoja na kuwepo kwa watu wawili wanaotumia cheti kimoja katika mfumo wa ajira. Ikumbukwe kuna ajira binafsi na serikalini ambao hawatumii data base moja kutunza taarifa za wafanyakazi wao hivyo inakuwa vigumu kudhibiti suala hili
Suluhisho la kudumu ni lipi? Karibu ndugu kuchangia mada hii. Elewa kuwa sababu za kupoteza cheti wakati mwingine inaweza kuwa ni kwa majanga au hata ajali. Ni kitu ambacho kamwe huwezi kupanga wala kudhani itatokea. Kama usivyojua siku yako ya kufa ndivyo usivyojua kesho yako. Waweza jikuta upo katika uhitaji. Nini kifanyike?
Nawasilisha hoja. Karibu kwenye mjadala huu: Shiriki kwa njia moja kati ya hizi unayoona ni rahisi kwako:
- Tumia sehemu ya maoni iliyopo chini ya habari hii.
- Facebook pages: Maganga Media na Students Resources Centre
- Facebook Group: MagangaMedia
- E – Mail: profmaganga@gmail.com
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII