HABARI MPYA LEO  

CAG: Mawaziri wapya msicheze!

By Maganga Media - May 7, 2012


ASEMA ATAWAKAGUA NA KUTOA RIPOTI KATIKA VIPINDI VITATU, VIGOGO WENGINE 'WAPUMULIA MASHINE'

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh amewaonya mawaziri wapya na watendaji serikalini kwamba ripoti zake hivi sasa zina nguvu za kusimamia uwajibikaji hivyo, wanapaswa kusimamia vyema wizara zao kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma.

Kauli hiyo ya Utouh ni ya kwanza tangu ripoti yake ya mwaka huu kuwang’oa mawaziri sita kati ya wanane ambao wizara zao zilionekana kugubikwa na ufisadi wa fedha za umma.

Akizungumza jana, Utouh alisema mawaziri wanapaswa kufahamu kwamba kuanzia sasa hadi mwaka 2015, zitatoka ripoti nyingine tatu, hivyo ni vyema wakachukua tahadhari wakiwa ndiyo wasimamizi wakuu wa shughuli za wizara.

Alisema kilichotokea bungeni na hadi mawaziri kuwajibishwa, kimethibitisha kuwa sasa kutakuwa na uwajibikaji mkubwa utakaosababishwa na ripoti zake kama watendaji wasipofuata taratibu za Serikali.

“Mawaziri ni wasimamizi wa wizara hata kama ni wanasiasa, wao ndiyo wanaowajibika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri wizarani hivyo ni muhimu wakafanya hivyo,” alisema Utouh.

Alisema kilichotokea ni sehemu ya uwajibikaji na kusema hatua iliyochukuliwa na Rais imetokana na ripoti ya ofisi yake kuonyesha udhaifu katika usimamizi uliofanywa na watangulizi wao hivyo kuwataka kuwa makini.

Utouh alisema kwa kuwa ofisi yake inapaswa kuandaa ripoti tatu hadi kufikia mwisho wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete watendaji hao waandamizi wa Serikali wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutimiza wajibu wao.

Alisema angalizo hilo haliwahusu mawaziri tu, bali hata watendaji walioko chini yao.

CAG alisema hivi sasa ofisi yake inaandaa ripoti nyingine mahsusi kuhusu vitendo vya jinai, rushwa na ubadhirifu vilivyotokana na kile kilichowang’oa viongozi hao tayari kwa ajili ya kuiwasilisha kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).

“Barua ambayo Takukuru walituandikia kuhusu wale ambao wamezungumzwa kwenye ripoti nimeiona na tunaishughulikia lakini nikwambie tu kwamba hata kama wasingetuandikia tungewapelekea kwa kuwa tumekuwa tunafanya kazi nao kwa karibu,” alisema.

Ripoti hiyo ya CAG ndiyo iliyamlazimu Rais Kikwete kupangua Baraza lake la Mawaziri na kuwang'oa sita, Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Nafasi za mawaziri hao sasa zimejazwa na Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Hussein Mwinyi (Afya na Ustawi wa Jamii) na Balozi Hamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).  

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII