HABARI MPYA LEO  

Askari waasi DRC wakimbilia Uganda

By Unknown - Jul 6, 2012

Askari wa Kongo wamekimbilia na kuingia nchini Uganda kufuatia mapigano na waasi, wakazi wa mji wa mpaka wa Bunagana wameiambia BBC.

Wenyeji Bunagana wamesema kuwa askari wengi walikuwa wamevuka mpaka, ambapo walipokonywa silaha na jeshi la Uganda .

Inaamikia kuwa waasi wemeudhibiti mji huo kwa upande wa Kongo ambao pia upo upande wa Uganda.

Waasi wa Bosco Ntaganda walibeba silaha na kuanza mapambano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Aprili.

Waasi hao ni wale waliojiondoa katika jeshi baada ya shinikizo kuongezeka kwa serikali kumkamata Jenerali Ntaganda, ambaye ni mshitakiwa wa uhalifu wa kivita anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya ICC.

Vyanzo vya habari kutoka Idara ya Usalama vimemwambia mwandishi wa BBC Ignatius Bahizi nchini Uganda kwamba waasi wa M23 wanadhibiti 15km wakizidi kushika kasi kuelekea mpaka wa kusini mwa mbuga maarufu ya wanyama ya Virunga "Virunga National Park" eneo lenye aina ya sokwe wanaishi milimani.

Wakazi wa Bunagana wanasema askari wa Kongo wamekuwa wakielekea mji wa Kisoro, ambao ni kilometa 80 kutoka mpakani.

Msemaji wa M23 Vianney Kazarama ameliambia shirika la habari AFP kwamba waasi wameushikilia mji huo kwa upande wa Kongo mapema siku ya Ijumaa habari ambazo pia zimethibitishwa na wakazi wa upande wa mji huo sehemu ya Uganda .

"Waasi hao wameudhibiti mji mzima ambapo watu wote na askari wa Kongo wapo Uganda." Chanzo cha polisi katika eneo hilo limeiambia AFP.

Karibu watu wapatao 200,000 wameyakimbia makazi yao baada ya mapigano ya hivi karibuni nchini Kongo, ambapo pia inasadikiwa watu 20,000 wamevuka mpaka kuingia Uganda na Rwanda.

Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitoa ripoti ikiituhumu nchi ya Rwanda kuwaunga mkono Waasi wa Jenerali Ntaganda ambao wengi ni Watutsi ambalo ndilo kabila la uongozi wengi wa Rwanda.

Hata hivyo nchi ya Rwanda ilikanusha madai hayo kwa nguvu zote.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII