HABARI MPYA LEO  

Mhadhiri anaswa na mtambo wa vyeti bandia

By Maganga Media - May 17, 2012

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamhoji mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (Muccobs), kwa tuhuma za kukutwa na vyeti vya kughushi vya vyuo vikuu kadhaa kwenye kompyuta yake.

Kukamatwa kwa mhadhiri huyo (jina tunalihifadhi), kumekuja siku chache baada ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kuibua tuhuma nzito za kuwepo askari 948, katika Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wenye vyeti bandia vya elimu.

Habari za uhakika kutoka Polisi na Muccobs, zinasema tayari kompyuta ya mhadhiri huyo ambayo ilikutwa na sampuli za vyeti hivyo, inashikiliwa na jeshi hilo kitengo cha makosa ya kughushi.
Taarifa hizo zimeeleza kuwa vyeti hivyo ni vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) Mwanza, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) Morogoro na ‘transcript’ za Muccobs.

Kukamatwa kwa mhadhiri huyo, kumekuja pia wakati kukiwepo kwa taarifa za kuzagaa kwa vyeti bandia vya Muccobs hususan ngazi ya stashahada ambavyo vinadaiwa kuuzwa kama njugu na mtandao mmoja ndani ya chuo hicho.

“Maneno yamekuwa mengi sana juu ya kuwapo kwa watu walioajiriwa katika taasisi mbalimbali nchini wakitumia vyeti vyetu, lakini hawajawahi kumaliza hapa kwetu,” alidokeza mhadhiri mmoja wa Muccobs.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Faustine Bee alithibitisha kukamatwa kwa mhadhiri huyo lakini akasema asingependa kulizungumzia jambo hilo kwa undani kwa kuwa linachunguzwa na polisi. 

KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII