HABARI MPYA LEO  

Shibuda atetea Uamuzi wake wa kugombea Urais

By Maganga Media - May 17, 2012

MBUNGE wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda ameeleza kuwa aliamua kutangaza nia ya kugombea urais Chadema kupitia vikao vya CCM kwa sababu anatambua kuwa hakuna mwanachama wa chama chake anayeweza kuwa Rais bila kuchaguliwa na chama hicho tawala.

Hata hivyo, jana Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limemshukia na kumtaka aeleze anafanya nini katika chama hicho kama anaamini kuwa hakiwezi kushika dola.

Shibuda alikaririwa na vyombo vya habari jana akieleza kuwa anataka kugombea urais kupitia Chadema na kumwomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwa meneja wake.

Jana, alipotakiwa kufafanua zaidi mantiki ya kauli yake hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) mjini Dodoma, Shibuda alisema anataka kuwa Rais wa Watanzania wote hivyo, hata kura za CCM anazihitaji ndiyo maana akatangaza mbele ya jukwaa lao.Shibuda alisema hakuna mwanachama wa Chadema anayeweza kuwa Rais wa nchi hii bila kupata kura za baadhi ya wanachama wa CCM na Watanzania wengine: “Hata katika hayo majimbo ambayo Chadema tumeshinda, hatukupigiwa kura na wanachama wa Chadema pekee, bali walikuwepo hadi wa CCM wanaopenda mageuzi.

"Mimi ni ‘field marshal’ katika siasa. Ndiyo, nimetangaza mbele ya jukwaa la CCM kwa sababu nahitaji kura zao. Nahitaji kura ya Kikwete na wana CCM wengine, mimi siyo mtu mwoga wa kutangazia vichochoroni Kariakoo," alitamba Shibuda na kuongeza:

“Mtu pekee mwenye boresho la kisiasa ni Shibuda. Mimi ndiye ninayeweza kujenga umoja na kutimiza malengo ya nchi. Ndiyo maana nilimwambia Rais Kikwete sasa ni zamu yangu na nitakangaza mbele ya jukwaa la CCM siyo kujificha vichochoroni Kariakoo.”

Shibuda akitetea msimamo wake, alisema si dhambi kwa mhadhiri wa Kiislamu kwenda kutoa mahubiri ya kutoa uchafu wa roho mbele ya jukwaa la Wakristo vivyo hivyo, kwa mhadhiri wa Kikristo kwenda kutoa mahubiri kwenye jukwaa la Waislamu na kuhoji: “Kuna uharamu gani au je, ni usaliti kwa dini yake?”

“Tuache fikra finyu. Shibuda anataka kuwa Rais wa Watanzania wote. Wanaosema kwa nini nimeongea kwenye jukwaa la CCM wana fikra finyu. Mimi nina maono mapana ya kitaifa. Kwani hata watu waliotalakiana bado wanashirikiana kwenye misiba na harusi, wanakutana na kusalimiana na hawana ugomvi wowote, hao ndiyo watu wastaarabu. Tuache kuzusha mambo kwa hisia hasi.”

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII