HABARI MPYA LEO  











Kesi ya mauaji ya marehemu Steven Kanumba inayomkabili movie star wa Tanzania Elizabeth Michael (Lulu) imeendelea kutajwa katika mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam huku suala la umri wa mshitakiwa huyo likiendelea kuwekwa kiporo.

Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu AUGUSTINA MMBANDO, Wakili wa Serikali KENNETH SEKWAO amesema upelelezi bado haujakamilika na kwa sasa ipo katika hatua ya kutajwa.

Mapema baada ya LULU kufunguliwa mashitaka ya mauaji ya msanii mwenzake STEVEN KANUMBA April mwaka huu, mawakili wanaomtetea waliwasilisha hoja ya kupinga umri wa mshitakiwa huyo na kutaka achukuliwe kama mkosaji mtoto kutokana na umri wake kuwa chini ya miaka 18 hali iliyolazimu suala hilo kupelekwa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoamua kulirejesha jambo hilo kwenye mahakama ya Kisutu.

Pamoja na kurejeshwa kwa suala hilo katika mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kumekuwa na ukimya wa muda sasa, kesi ya LULU imeahirishwa mpaka Disemba 17 mwaka huu ambapo itakwenda kwaajili ya kutajwa.
Maelfu ya Walibya wamefanya mhadhara katika mji wa Benghazi, mashariki mwa Libya, kuunga mkono demokrasi na kuwapinga wapiganaji wa Kiislamu.
Maandamano ya kupinga wapiganaji mjini Benghazi
Waandamanaji waliisihi serikali ya Libya iyapige marufuku makundi ya wapiganaji ambao wamekataa kukabidhi silaha zao tangu vita dhidi ya Kanali Gaddafi mwaka jana. Waandamanaji wanataka serikali izidishe jeshi na polisi, na walimsifu balozi wa Marekani aliyeuliwa mjini humo juma lilopita. Waliimba wakati wakiandamana kuelekea medani kuu ya Benghazi.

Muandamanaji mmoja, Faisla al-Naas, alieleza sababu zao: "Sisi tunaandamana kupinga kundi lenye silaha ambalo halidhibitiwi na serikali. Wapiganaji hawa wanafaa kujiunga na serikali ili watu wakae kwa salama.
Nchi yetu imekuwa na mtafaruku."

Maandamano mengine ya kuunga mkono wapiganaji yalikuwa madogo sana.
DUNIA haikaukiwi matukio ya kustaajabisha, kwa hakika huu ni ulimwengu maridhawa na hawakukosea walionena kwamba dunia hadaa ulimwengu shujaa.
 
Stori ya kusikitisha, inatokea nchini Marekani ambako kijana Justin Street, amepoteza maisha akiwa kwenye jaribio la kuongeza ukubwa wa nyeti yake.


Habari kamili ipo hivi; Justin, 22, akiwa baba wa watoto wawili alikwenda kwa mwanamama Kasia Rivera ,35, aliyejitangaza kuwa ni mtaalamu wa tiba za kuongeza ukubwa wa nyeti za kiume.


Kasia aliweka matangazo barabarani kuwa anayo tiba ya kuongeza ukubwa wa nyeti za kiume, hivyo kumfanya Justin ahamasike kwenda kupata dawa hiyo ili kujiongezea ushababi. 


Wanasema tamaa mbele mauti nyuma, ndivyo ilivyotokea kwa Justin, kwani baada ya kuomba dawa ya kuongeza ukubwa wa maumbile yake ya kiume, alidungwa sindano yenye madini ya silikoni.


Madini hayo, alidungwa kwenye nyeti yenyewe na baada ya muda mfupi, hali ya afya yake ilibadilika kuwa mbaya, alizorota na siku iliyofuata alifariki dunia.


Kutokana na tatizo hilo, Kasia alifikishwa mahakamani kwa kesi ya mauaji akituhumiwa kufungua zahanati bubu ndani ya nyumba yake iliyopo New Jersey, vilevile kutoa tiba za kiafya wakati hana taaluma hiyo wala leseni ya kuendesha kazi hiyo ya utoaji huduma za afya.


Kasia alipandishwa kizimbani wiki iliyopita, uchunguzi wa maiti umethibitisha kwamba Justin alifikwa na mauti baada ya madini ya silikoni aliyodungwa kwa sindano kuziba njia za mishipa ya damu.


Mmoja wa madaktari waliomfanyia uchunguzi Justin alisema kuwa hii ni mara ya kwanza kusikia silikoni inayotumika kuongeza ukubwa wa matiti ya wanawake imetumika kwenye kuongeza ukubwa wa uume.Kasia, amekana kuhusika na mauaji hayo.


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewavua madaraka wakurugenzi sita wa Halmashauri za Wilaya kwa kushindwa kusimamia rasilimali watu, fedha na kutowajibika.

Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mkuu Pinda amewateua watu sita kukaimu nafasi hizo na wakurugenzi wapya 14 huku akiwahamisha wakurugenzi 27 kutoka katika vituo vyao vya kazi kwa sababu mbalimbali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Hawa Ghasia, alisema wakurugenzi hao walivuliwa madaraka kwa kushindwa kusimamia rasilimali watu na fedha, kusababisha halmashauri kupata hati chafu na uzembe.

Aliwataja wakurugenzi hao waliovuliwa madaraka kuwa ni Willy Njau (Mwanga), Mpangalukela Tatala (Geita), Theonest Nyamhanga (Kishapu), Eden Munisi (Morogoro), Mhando Senyagwa (Kyela) na Nicholaus Kileka (Ngorongoro).

Pia alisema Serikali haitasita kuchukua hatua pale inapobidi ili kuboresha utendaji, na kwamba wengine tayari wana kesi na si busara kuwe na mtu anayekaimu zaidi ya miaka mitatu.

Pia alisema hatua za kinidhamu bado zinaendelea na kwamba baadhi ya wakurugenzi hao tayari wamewafikisha kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya hatua zaidi.

Waziri huyo aliwataja wakurugenzi wapya walioteuliwa kujaza nafasi hizo kuwa ni Abdalah Kidwanka (Geita), Rutius Bilakwata (Kishapu), Naomi Nko (Magu ), Abdalah Mfaume (Kyela), Twalib Mbasha (Monduli), Henry Ruyagu (Urambo), Adam Mgoyi (Mbarali) na Estomih Chang’a (Mpanda).

Wamo pia Leti Shuma (Mwanga), Mohamed Maje (Namtumbo) Fulgency Mponji (Moshi), Robert Nehata (Tunduru), Isabela Chilumba (Kahama), Fikiri Malembeka (Sengerema), Paul Malala (Njombe) na Nasib Mbaga (Biharamulo).

Wakurugenzi wanaohamishwa ili kujaza vituo wazi ni Bibie Mnyamagola (Kongwa), Daudi Mayeji (Kilindi), Protace Magayane (Nkasi), Saada Mwaruka (Mkuranga), Sipora Liana(Tabora Manispaa), Hadija Makuwani (Wilaya ya Tabora), Doroth Rwiza (Kasulu).

Wengine ni Kelvin Makonda (Manispaa ya Lindi), Pudenciana Kisaka (Iringa), Tina Sekambo (Makambako), Beatrice Dominick (Masasi), Gladyness Ndyamvuye (Bukoba), Nathan Mshana (Ngorongoro), Cornel Ngudungi (Ngara), Mohamed Mkupete (Mtwara Manispaa), Dk Koroine Ole Kuney (Misungwi).

Wamo pia Ephraem Ole Nguyaine (Rorya), Goody Pamba (Igunga), Fidelis Lumato (Ludewa), Athuman (Tarime) na Ahmad Sawa (Musoma Manispaa).

Waliohamishwa kwenda kwenye halmashauri mpya ni Magreth Nakainga (Geita), Eliza Bwana (Bariadi), Zuberi Mbyana, Ilemela Manispaa (Biharamulo), Mohamed Nanyanje (Masasi), Erica Musika (Kahama), Imelda Ishuza (Busokelo).

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari

Juzi malori 30 yaliyokuwa yamejaa sarafu (ama kunogesha zaidi chenchi) za senti tano tano, yaliwasili kwenye makao makuu ya Apple, jimboni California, Marekani.

Awali, walinzi wanaolinda makao hayo makuu walidhani malori hayo yamepotea njia, lakini dakika chache baadaye, Tim Cook (CEO wa Apple) alipokea simu kutoka kwa CEO wa Samsung Lee Kun-hee, akimueleza kuwa wamewalipa faini yao ya dola bilioni 1, kutokana hukumu dhidi ya kampuni hiyo ya Kikorea.
Tim Cook
Kitu cha kuchekesha zaidi ni kuwa nyaraka iliyosainiwa haioneshi njia moja ya kulipa faini hiyo, hivyo Samsung ilikuwa na haki ya kuwapelekea faini hiyo watengenezaji hao wa simu za iPhone vyovyote wanavyotaka.

Lee Kun-hee
Mchezo huu mchafu na wa kijanja utawaumiza kichwa wakurugenzi wa Apple kwakuwa itabidi iwachukue muda mrefu kuhesabu fedha zote ili kuhakikisha kama zimetimia na kujaribu kuzipeleka benki ambako hawajui kama zitakubalika.

Mwenyekiti wa Samsung Electronics Lee Kun-hee, amewaambia waandishi wa habari kuwa kama Apple wanataka kucheza mchezo mchafu na wao pia wanaujua. Undava undava na kama noma iwe noma tu!
Wendesha mashtaka wa serikali nchini Afrika Kusini wanasema kuwa wanajianda kuwafungulia mashtaka ya mauaji wachimba migodi wa mgodi wa Marikana.  Ripoti zinasema pia, wachimba migodi hao, wanakabiliwa na mashtaka mengine ikiwemo jaribio la mauaji ya wachimba migodi thelathini na wanne ambao waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Msemaji wa ofisi ya kiongozi wa mashtaka nchini humo, amesema ikiwa watu, ambao baadhi yao wamejihami wakiwakabili polisi na kutokee mauaji, wale watakaoshikwa na polisi watafunguliwa mashtaka ya mauaji, bila kujali wale waliofyatua risasi.

Polisi waliwapiga risasi wachimba migodi hao kufuatia ghasia na maandamano kuhusu mishahara.
Maafisa wawili wa polisi waliuawa kwenye machafuko hayo.
Kwa niaba ya TANESCO na kwa faida ya wasomaji wangu wa Maganga Media, nimesikiliza kipindi cha TANESCO na MAENDELEO kinachorushwa na TBC1 leo asubuhi na kukutana na taarifa hii ambayo sidhani kama kila mtu anayo.

Ni kuwa TANESCO wameamua kuboresha system ya mita za luku kote nchini kuanzia Tarehe moja Septemba. Kwa mteja wa TANESCO anayetumia mita ya LUKU anatakiwa kama luku yake itaisha baada ya Tarehe 1.9.2012 ANATAKIWA KWENDA KUNUNUA LUKU KATIKA VITUO VYA MAUZO YA LUKU VYA TANESCO ili alipie luku yake. Hapo atapewa risiti 3, Mbili zikiwa ni za utambuzi na marekebisho ya mfumo wa LUKU na hiyo ya 3 ndio ya TOKEN (Umeme ulionunua). Zingatia uende kwenye kituo cha TANESCO, sio lazima uende ofisini, vipo hata mitaani kwa miji mikubwa vimeandikwa TANESCO OFISI YA MALIPO.

Kwa mujibu wa mzungumzaji wa kipindi hicho, sio kwamba wanasitisha njia zingine za kununua umeme kama kwa kupitia njia ya simu, ATM, MAX, na njia nyingine unazoona ni rahisi kwako, bali wanaboresha tu kwa ajili ya manufaa. Mteja kwa mara ya kwanza kuanzia mwezi wa tisa tarehe mosi akinunua umeme kwa njia nyingine umeme huo hautasoma kwenye mita yako ya LUKU. Ukienda TANESCO umeme huo uliolipia utarudishiwa (pesa yako haipotei) ila kukwepa usumbufu, ni bora ukanunue katika ofisi za mauzo za TANESCO.

Ushauri alioutoa ni kuwa si lazima wote mkimbie na kwenda ofisi za TANESCO ifikapo tarehe moja, ila kama utakuwa na UNITS zako utaendelea kutumia hadi zitakapoisha. Muhimu ni yeyote atakayenunua UNITS ZA LUKU kuanzia tarehe moja akanunue katika vituo vya malipo vya TANESCO. Baada ya hapo ndipo utaendelea na utaratibu wako wa kununua katika njia uliyozoea wewe kama ni, ngoja nizitaje kwa hisani yao, (siwapigii debe wenye mitandao hiyo, ni kwa faida ya jamii) kuna MPESA, TIGO PESA, NMB ATM NA NMB MOBILE, MAXCOM, NK.

MAULIZO: 0768 985 100, 022 219 4400
 
KWA MASWALI TEMBELEA KITUO CHA TANESCO KILICHO KARIBU NA WEWE. KAMA BADO KUNA KITU HUJAKIELEWA VIZURI, INGIA KWENYE SANDUKU LA MAONI HAPA CHINI NA ULIZA SWALI LAKO UTAJIBIWA. HII ITAKUSAIDIA SANA KULIKO KWENDA OFISINI MOJA KWA MOJA WAKATI MAJIBU YAPO. Mwisho wa TANGAZO.

TANESCO, wanayaangaza maisha yako!
MAMLAKA ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema umri wa madereva wa Usafiri wa Umma unapaswa kuanzia miaka 30 hadi 60 ili kuepusha ajali za mara kwa mara.

Hatua hiyo imekuja wakati kukiwa na matukio mengi ya ajali ambazo zinahusishwa na uzembe wa madereva na kutozingatia sheria za barabarani.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa barabarani, Aron Kisaka wakati akiwasilisha Kanuni za leseni ya usafirishaji kwa magari yanayotoa huduma ya usafiri wa umma ya mwaka 2012 kwa wadau wa usafiri.

Vipengele vingine vilivyo wasilishwa katika Kanuni hizo ni pamoja na dereva kutoruhusiwa kuendesha gari zaidi ya saa nane mfululizo, kuendesha gari huku akiongea na simu pamoja na kuendesha gari huku akiwa ametumia kilevi cha aina yoyote.

SOMA ZAIDI KWA KUCLICK HAPA: GAZETI LA MWANANCHI

SIO UJANJA BALI NI UJINGA NA KUJICHIMBIA KABURI KWA KUSHINDWA KULIPA SH 200/= KAMA NAULI YA DALADALA KUTOKA NJIA PANDA YA KIGOGO HADI MIKUMI ( MAGOMENI) JIJINI DAR ES SALAAM. TUKIO LIMETOKEA MWISHONO MWA WIKI. PICHA NA MDAU WETU.


UNA KERO YOYOTE? TUTUMIE. E_MAIL: profmaganga@gmail.com
Mtu mmoja anadaiwa kufa kwa kupigwa risasi Kichwani huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya kwa Risasi za moto baada ya Polisi kuwarushia Risaasi za moto na mabomu ya machozi waandamani wa Chadema mjini hapa.

Baadhi ya wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA mkoani Morogoro wakiongozwa na polisi baada ya kuwatawanyisha walipokuwa wakifanya maandamano maeneo ya Msamvu mjini Morogoro mchana wa leo. Polisi walitibua maandamano hayo yanayodaiwa kutokua rasmi kwa mabomu ya machozi.
 Huyu ni Ally Zona muuza magazeti wa Msamvu Morogoro akiwa hajitambui baada ya kutandikwa risasi na Polisi kuzuia maandamano ya chadema

SOURCE-father kidevu
Hii ni matokeo ya kudumisha mila na desturi za kurithiana.

Mama Condorada Ngonyani mwenye umri wa miaka 70 anaishi kinyumba kama mke na mume na mwanaye wa tatu wa kumzaa mwenyewe akidai kuwa mara baada ya kufariki mume wake, Mzee Mapunda alimchagua mtoto wake amrithi baba yake.

Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia na wtoto kuangalia kati sheria inayomruhusu Mtoto na Mama Mzazi kuweza kuishi kindoa


Umati wa watu wapatao 400 ulifurika kwa Mganga wa Jadi Flora Ndembo Namabengo wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma wakiiomba Serikali ichukue Mkondo wa Sheria dhidi ya condorada ngonyani na joseph Mapunda.


Joseph Mapunda mwenye umuri wa miaka 40 amesema ameweza kuishi kindoa na Mama yake Mzazi Condorada Ngonyani 70 baada ya yeye kukubaliana wenyewe yeye na mama yake mzazi kuishi kindoa kama mume na mke.

Alipo ulizwa Mama alikiri kuwa kweli wameishi kindoa kwa miaka 10 na anampenda Mume wake ambaye ni Mtoto wake Joseph Mapunda.
Mama Condorada Ngonyani mwenye umuri wa miaka 70 ambaye ana ishi kinyumba na mtoto wake watatu wa kumzaa mwenyewe kama Mke na Mume hapo anaonekana akisononeka kwa nini jamii iingilie ndoa yake
Kwa mkoa wa Ruvuma hii ni mara ya kwanza mtoto wa kiume Joseph Mapunda pichani hapo juu kutembea na mama yake mzazi. 
Wana Ruvuma wanauliza tume jikwaa wapi watanzani hadi kupoteza mila desturi na maadili ya mtanzania pia kukiuka sheria za dini
Joseph Mapunda ana sema upendo ni upendo amempenda mama na anaishi kindoa wamependana nyie watu mnataka nini kwetu ?
Mama Condorada Ngonyani anasema mara baada ya kufariki mume wake Mzee Mapunda alimchagua mtoto wake amrithi baba yake
Ndugu wananchi;

Ndugu wananchi;
Imekuwa ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.  Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu maalum.  Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo.  Naomba kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.

Ndugu wananchi;
Katika historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964.  Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002.  Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati  wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na  1957.  Kwa upande wa Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.

Ndugu Wananchi;
Kama ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu,  mahali walipo, jinsia zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.  Aidha, huisaidia Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika.  Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili.  Vilevile, takwimu hizi hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji vipya.

Ndugu wananchi;
Pamoja na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu,  Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake.  Taarifa zake zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na Zanzibar;  Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini  Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka 2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.

Ndugu Wananchi;
Pamoja na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi  yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.

Ndugu wananchi;
Shughuli yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida.  Lakini, tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kuwepo.  Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya jitihada za makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini.  Wamekuwa wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo baadhi yake hazina uhusiano wo wote na Sensa.  Zipo sababu nyingine ambazo hata haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa hawatashiriki Sensa mpaka mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule Berlin, Ujerumani atakaporudishwa.  Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa nchini zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita.  Mwaka 1906 wana sayansi wa Kijerumani waliyagundua mabaki hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na kuyapeleka Ujerumani ambako yamehifadhiwa tangu wakati huo.

Ndugu Wananchi;
Kudai mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa kale waliokuwepo wakati huo wanafananaje.  Huenda pia kikawa kivutio cha utalii.  Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi.  Watu wakisusia Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali hata watu wengine nchini na duniani watawashangaa.  Lakini, jambo ambalo ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani?  Mjerumani au wanajisusia wenyewe?  Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata akirejeshwa huna manufaa ya moja kwa moja?  Hasara anapata nani sisi au wao?  Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza maneno yahusuyo Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa mambo yenye maslahi makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu.  Tuachane nao hawatutakii mema na wala hawaitakii mema nchi yetu.  Nawaomba tusitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni.

Ndugu Wananchi;
Wapo ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika orodha ya maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu.  Wahusika wakuu hasa ni baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu wasikubali kuhesabiwa.  Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi Waislamu wawaunge mkono katika msimamo wao huo.  Nimesoma baadhi ya nyaraka na vipeperushi vyao kuhusu madai hayo.  Nilipata pia bahati ya kukutana na kuzungumza na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati hizo.  Nia yangu katika kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani hoja na madai yao.  Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki, Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania.

Hawazikubali taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji wa takwimu hizo.  Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya kuwa ni asilimia fulani Watanzania.  Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu.  Kwa maoni yao, taarifa hizo si za kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu wanazozijua watoaji wa taarifa hizo.  Ili kuondoa upotoshaji huo, wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.

Katika mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo.  Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika hayo.  Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya watu hutolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha Serikali.  Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na wala siyo chanzo cha takwimu zilizotolewa na mashirika hayo.  Walikozipata wanajua wenyewe.  Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na ndiyo maana zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na wakipenda watoe tamko la kuzikataa.

Ndugu Wananchi;
Niliwaambia pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni kuionea na kutoitendea haki.  Vile vile  kuibebesha dhima ya kuongeza swali la dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili.  Napenda, kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna hiyo kutambua unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea mifarakano isiyokuwa ya lazima kama ilivyo sasa.

Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya kuliingiza swali la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na kiutekelezaji.  Wakati wa ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu yaliulizwa katika Sensa.  Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika Sensa ya kwanza ya mwaka 1967 kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya kikoloni.  Baada ya hapo ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza maswali hayo kwani nia ya wakoloni kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale.  Walitoa huduma kwa ubaguzi, sera ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na Mapinduzi.  Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, bali kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.

Ndugu Wananchi;
Sera hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa letu na watu wake.  Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni wengi na hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa, sera mpya inawataka watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.

Ndugu Wananchi;
Nionavyo mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima kubwa.  Tuendelee kuidumisha na kuienzi.  Kufanya vinginevyo,  na hasa kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu  ni kuliingiza taifa letu ambalo lina sifa ya  amani, upendo na utulivu, katika migogoro isiyokuwa ya lazima.  Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na kudumisha sera yetu hii  nzuri na sahihi.

Ndugu Wananchi;
Sababu ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji.  Imechukua miaka kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.  Isitoshe Sensa ya majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali yaliyopo na marekebisho kufanywa baada ya hapo.  Kuingiza mambo au jambo jipya sasa itakuwa viguku kiutekelezaji.  Kutachelewesha zoezi zima na kusababisha hasara kubwa kwa taifa.

Kwa vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo cha kutoa huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu wanaokereketwa na jambo hili waache kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze kuhesabiwa. Tujitokeze kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya wananchi wa Tanzania.

Ndugu Wananchi;
Sioni ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo na Waislamu.  Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi Kuu ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo.  Hata ukiamua uiite Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana sababu.  Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa msingi wa dini kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na Waislamu.   Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.

Ndugu Wananchi;
Katika maelezo yao kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Said na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa walinieleza kwamba kwa kawaida katikati ya Sensa moja na nyingine, hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani Demographic Survey.  Huu ni utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya kaya ambapo taarifa za mambo mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa hukusanywa.  Mara ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973, yaani baada ya Sensa ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978.  Ni makusudio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016 ambapo baadhi ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa.  Subira yavuta heri.

Ndugu Wananchi;
Nimehakikishiwa na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri na zoezi liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012. Lakini, mafanikio ya zoezi lenyewe  yatategemea sana ushiriki wa watu ambao ndiyo walengwa na wadau wengine.    Naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa kisiasa na kiutendaji wa ngazi mbalimbali waendelee  kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika maeneo yao ya uongozi.  Hawana budi kuhakikisha kuwa zoezi linakuwa na mafanikio makubwa.  Wale wote wanaofanya vitendo vya kuvuruga zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
Nawaomba viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na kushirikiana na Makarani wa Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao.  Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi wasijitokeze kuhesabiwa.  Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema nchi yetu.

Ndugu wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi wa kisiasa, kusimamia na kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Sensa katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji  na Shehia kwa kazi nzuri ya matayarisho na uendeshaji wa Sensa ya mwaka 2012.  Nawatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu na adhimu kwa nchi yetu na watu wake.

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu hawa kwa kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012.  Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza kwetu ndiyo ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.  Ewe Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa   kwa maendeleo yako na ya taifa letu.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa kunisikiliza
Open your account today. All dues has been payed by Jesus Christ. Through his death we all set free. To run the account is so simple as there is neither monthly costs nor withdraw charges, what you have to do is to maintain your relationship with God. Good Sunday to every one!

Maandiko:
Rom 3:23 - All have sinned
2Cor 6:2 - Wakati wa wokovu ni sasa
John 3:16 Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwana wake wa pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.
Rom 6: 23 - Mshahara wa dhambi ni mauti lakini atoacho Mungu kupitia Yesu Kristo ni uzima wa milele.
Rom 5:8 Tulipokuwa wenye dhambi Yesu alitufia 
Yoh 1:12 - Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu.

MSIBA wa aliyekuwa staa wa muvi za Kibongo, Steven Kanumba umeanza upya kwenye Kijiji cha Izigo, Muleba, Kagera baada ya mama mzazi wa marehemu, Flora Mtegoa kuupeleka msiba huo huko sanjari na mchanga wa kaburi la Dar. Akizungumza kwa masikitiko  makubwa, mama wa Kanumba alisema tangu kifo cha mwanaye hakuwahi kupeleka msiba kijijini kwake kama mila na desturi zinavyotaka.

Aliongeza kuwa hiyo yote ilitokana na kukosa muda kwani licha ya mazishi, bado watu mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi walikuwa wakiendelea kumiminika nyumbani kwake kwa lengo la kumfariji. Alisema kuwa alipofika Kagera, alipokelewa na umati wa waombolezaji na msiba ulianza upya, jambo ambalo hakulitarajia.
“Nilipofika kijijini nilipokelewa na ndugu, jamaa na marafiki, kwa kweli msiba ulianza upya. Sikutarajia, watu walilia na kuomboleza,” alisema mama Kanumba.

Akaongeza: “Kwa kweli kutokana na hali ilivyokuwa, hata mimi mwenyewe nilijikuta nalia sana. Nilihisi siku hiyo ndiyo mwanangu alifariki dunia rasmi kwa jinsi watu walivyokuwa wakiomboleza. Akaongeza tena: “Ilibidi tufanye mambo ya mila na desturi za Wahaya zikiambatana na kuzika mchanga niliouchota kwenye kaburi la Dar (Kinondoni). Mama Kanumba alisema anamshukuru Mungu walizika salama (mchanga) na kwamba muda si mrefu alitarajia kurejea jijini Dar kutoka kwenye msiba huo.

 “Namshukuru Mungu tumezika salama kwa kweli, mimi mwenyewe naendelea vizuri huku nikinywa dawa za Kihaya, nakaribia kurudi Dar hivi karibuni,” alisema mama Kanumba. Steven Charles Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa madai ya kusukumwa na Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambaye anashikiliwa na vyombo vya dola.

CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS
Raia 37 wa Uchina wamerejeshwa nyumbani kutoka Angola, ambako walikamatwa kwa tuhuma za kufanya uhalifu dhidi ya Wachina wenzao.
Wahalifu wa Kichina wakiwasili kwao kutoka Angola
Uhalifu huo ni pamoja na utekaji nyara, kunyang'anya watu pesa, wizi kwa kutumia silaha, na kulazimisha wanawake wauze miili yao. Kikosi maalumu cha polisi wa Uchina kilitumwa Angola kushirikiana na polisi wa huko dhidi ya magengi ya Wachina yaliomo Angola. Wizara ya Uchina ya usalama inasema magengi 12 yalivunjwa.

Wizara hiyo ilisema hii ni mara ya kwanza kwa polisi wa Uchina kufanya msako mkubwa kama huo dhidi ya wahalifu wa Kichina katika bara la Afrika.



“Namtaarifu Komredi Yusufu Makamba, kuwa yule kiboko yake 'MATONYA' amefariki usiku wa kuamkia leo kijijini kwakwe Mpamantwa wilaya ya Bahi, mazishi yamefanyika leo saa 10 jioni kijijini hapo. Habari ziwafikie, Mkuu wa Wilaya Betty Mkwasa, Familia ya Mzee Makamba popote walipo, wakazi wa Dar na Moro pamoja na ndugu jamaa na marafiki wote. Bila ya kusahau wale wa eneo la Darajani Mjini Morogoro”
 
CHANZO: THE CHOICE
Salim Kikeke Ndiye mtangazaji wa kipindi hiki.

 
                                                                       
BBC Idhaa ya Kiswahili kuzindua Dira ya Dunia kupitia Star TV nchini Tanzania

23 August 2012. Katika mpango mkubwa wa kutanua wigo wake wa wasikilizaji na watazamaji barani Afrika, BBC imetangaza kuzindua kipindi chake cha kwanza cha habari za dunia kwa lugha ya Kiswahili kiitwacho Dira ya Dunia. Kuanzia Jumatatu Agosti 27, kituo shirika cha BBC Idhaa ya Dunia nchini Tanzania, Star TV, kitarusha kipindi cha Dira ya Dunia cha BBC Idhaa ya Kiswahili. Matangazo hayo ni ya dakika 30 yakiwapa watazamaji fursa ya kupata habari motomoto za dunia na uchambuzi yakinifu kutoka katika shirika hilo la utangazaji la kimataifa ulimwenguni.

Kipindi hicho ambacho kitakuwa kikirushwa kila Jumatatu hadi Ijumaa kitatoa chachu katika matangazo ya Star TV kwa kuwaletea watazamaji habari za kiwango cha hali ya juu kutoka katika kitovu cha habari za dunia cha BBC- Global News. Dira ya Dunia pia itawaletea watazamaji taswira na uchambuzi yakinifu kutoka kwa waandishi wa habari waliotapakaa katika nchi 48 barani Afrika, na hivyo kuleta picha halisi ya bara zima kwa watazamaji wanaozungumza Kiswahili.

Kipindi cha radio cha Dira ya Dunia ni kipindi maarufu sana kwa mamilioni ya wasikilizaji katika eneo la Afrika Mashariki na Kati na hata wasikilizaji wanaoishi nje ya eneo hilo. Kwa kuzindua kipindi cha TV chenye jina kama hilo, BBC ina imarisha zaidi matangazo yake hasa kwa kutumia waandishi wake wa habari waliobobea – watangazaji Salim Kikeke na Charles Hilary, mhariri Mariam Omar pamoja na waandishi waliopo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na Uingereza.

Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Ali Saleh anasema: “Uzinduzi wa Dira ya Dunia kupitia TV, ni kwenda na mabadiliko makubwa tunayoyashuhudia ya jinsi watu wanavyofuatilia habari barani Afrika, na pia mahitaji wa mashabiki wa BBC Ihdaa ya Kiswahili. Tunavyoarifu na kuchambua habari za eneo letu na hata duniani, iwe siasa, uchumi au utamaduni, Dira ya Dunia itatoa taswira halisi ya Afrika, tofauti na jinsi ambavyo bara hili limekuwa likiripotiwa kwa miaka mingi. Kipindi chetu kitakuwa kinashirikisha watazamaji, na pia kuzigatia misingi ya BBC ya muda mrefu ya uhuru, uhakika na bila upendeleo”

Kinara wa Dira ya Dunia, Salim Kikeke ameongeza kwa kusema: “Ni heshima kubwa na nafasi ya kipekee kuwa katika mradi huu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC wa TV. Tumepitia mengi hadi kufika hapa, na kila sekunde ya safari hiyo ilikuwa ni ya kuvutia.Ni imani yangu kuwa kipindi hiki kipya cha TV kitavutia wengi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.”

Uanzishaji wa Dira ya Dunia katika TV ni sehemu ya mabadiliko makubwa ya matangazo yaliyofanyika ndani ya BBC mwaka huu katika bara la Afrika, katika TV na redio. Uzinduzi huu umekuja muda mfupi baada ya kuzinduliwa kwa kipindi cha TV kwa lugha ya Kiingereza kwa Afrika, Focus on Africa, ambacho pia kinarushwa kupitia Star TV. Mwezi Julai, siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Olimpiki jijini London, BBC Idhaa ya Ulimwengu ilizindua kipindi kipya cha redio, Newsday – Kipindi ambacho kimelenga zaidi wasikilizaji wa redio wa asubuhi barani Afrika.

Mhariri wa BBC wa eneo la Afrika, Solomon Mugera, naye amesema: “Miongo mingi ya utangazaji katika lugha mbalimbali barani Afrika, BBC imejenga uhusiano wa kipekee na wasikilizaji wetu wa redio, kwa kueleza ya Afrika duniani, na kuipeleka dunia barani Afrika. Kukua kwa njia za utangazaji za BBC ni ushahidi wa kuwepo kwa mizizi ya muda mrefu na ufahamu wa bara la Afrika. Tunavyoanza safari hii mpya, kwa kweli tuna hamasa kubwa hasa kwa kushirikiana na mashirika ya utangazaji yenye hadi kubwa katika eneo letu.”

Nathan Lwehabura, Meneja mipango na utafiti wa SMG Ltd, anasema: “ Ni heshima kubwa kwa Star TV kujumuisha Dira ya Dunia katika vipindi vyake vya kila siku – tunaamini kipindi hiki kitavutia watu wengi. Kipindi cha BBC cha Kiingereza kilichozinduliwa hivi karibuni kupitia Star TV, Focus on Africa, kinazidi kujipatia umaarufu mkubwa, sio tu miongoni mwa watazamaji wetu, bali pia hata miongoni mwa mashirika mengine kutokana na kuzingatia fani ya uandishi, utangazaji na ubora wa kipindi. Ni matumaini yetu kuwa ushirika kati ya BBC na Sahara Media Group utaimarisha matangazo yetu ya TV hasa tunavyoelekea katika matangazo ya kisasa ya mfumo wa digital.”

Dira ya Dunia kutoka Idhaa ya Kiswahili ya BBC itakuwa ikitangazwa Jumatatu hadi Ijumaa, saa tatu usiku kupitia Star TV nchini Tanzania. Pia matangazo hayo yatapatikana kupitia wavuti wa BBC Idhaa ya Kiswahili – bbcswahili.com.

BBC ilirusha matangazo yake ya kwanza kabisa barani Afrika zaidi ya miaka 80 iliyopita. Idadi kubwa ya wasikilizaji kwa ujumla kupitia redio na TV inaifanya BBC kuwa shirika kubwa zaidi la kimataifa la utangazaji barani Afrika.

Kwa taarifa zaidi tafadhali wasiliana na:

BBC Global News Press Office
+44 207 557 2944; sophie.west@bbc.co.uk


Kwa wahariri:

BBC Idhaa ya Kiswahili ni watangazaji wa habari kupitia TV, redio na kwenye mtandao kwa lugha ya Kiswahili na kwa wasikilizaji na watazamaji wa lugha hiyo. Matangazo ya redio kwa Kiswahili yanapatikana kupitia vituo vya redio vya FM na pia kupitia redio washirika nchini Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya, Malawi, Mozambique, Rwanda na Uganda. Matangazo pia yanapatikana kupitia wavuti bbcswahili.com ambapo pia habari mpya kabisa zinapatikana, makala na uchambuzi kuhusu Afrika Mashariki na pia duniani kote, kwa maandishi, sauti na video.

BBC Idhaa ya Kiswahili ni sehemu ya BBC Idhaa ya Dunia (BBC World Service), ambao ni watangazaji wa kimataifa wanaotoa huduma ya matangazo kwa lugha mbalimbali kupitia redio, TV na kwenye wavuti na pia kupitia vifaa vitumiavyo visiwaya. Kwa taarifa zaidi tembelea bbcworldservice.com

BBC ina mashabiki milioni 239 kwa wiki duniani kote katika huduma zake za habari za kimataifa ikiwemo BBC World Service, BBC World News TV na bbc.com/news.

IDHAA ya Kiswahili ya BBC imezindua kipindi cha habari cha Dira ya Dunia hapa nchini ambacho kitarushwa moja kwa moja kutoka Londonkupitia Kituo cha Televisheni cha Star(Star TV)
Kipindi hicho cha nusu saa kitakuwa cha kwanza duniani kutangazwa kwa Kiswahili kupitia televisheni ya Star Tv hapa nchini.

Mhariri wa BBC Idhaa ya Kiswahili, Ali Saleh alisema kipindi hicho cha nusu saa kitaanza kurushwa rasmi Agosti 27,mwaka huu kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa saa 3 usiku kupitia  Star Tv.

Saleh alisema kipindi hicho kitatoa chachu katika matangazo ya Star TV kwa kuwaletea watazamaji wa habari za kiwango cha juu kutoka katika kitovu cha habari za dunia cha BBC-Global News. “Uzinduzi wa Dira ya Dunia kupitia TV, ni kwenda na mabadiliko tunayoyashuhudia ya jinsi watu wanavyofuatilia habari barani Afrika, na pia mahitaji ya mashabiki wa BBC Idhaa ya Kiswahili,”alisema Saleh na kuongeza.

“Dira ya Dunia itawaletea watazamaji taswira na uchambuzi yakinifu kutoka kwa waandishi wa habari waliotapakaa katika nchi 48 barani Afrika, na hivyo kuleta picha halisi ya bara zima kwa watazamaji wanaozungumza Kiswahili”.
Huyu ndiye Salimu Kikeke, mtangazaji wa kipindi hicho

Alisema Dira ya Dunia itatoa taswira halisi ya Afrika, tofauti na jinsi ambavyo bara hili limekuwa likiripotiwa kwa miaka mingi. Kipindi chetu kitakuwa kinashirikisha watazamaji, na pia kuzigatia misingi ya BBC ya muda mrefu ya uhuru, uhakika na bila upendeleo.

Mpaka sasa BBC ina mashabiki 239 milioni kwa wiki duniani kote katika huduma zake za habari za kimataifa ikiwemo BBC World Service, BBC World News TV na bbc.com/news.

BBC Idhaa ya Kiswahili ni sehemu ya BBC Idhaa ya Dunia (BBC World Service), ambao ni watangazaji wa kimataifa wanaotoa huduma ya matangazo kwa lugha mbalimbali kupitia redio, TV na kwenye wavuti na pia kupitia vifaa vitumiavyo visiwaya. 

CHANZO: Mwananchi
Waombolezaji nchini Afrika Kusini
Waombolezaji nchini Afrika Kusini
Maelfu ya watu nchini Afrika Kusini wamehudhuria misa ya kuwaombea watu waliouawa katika machimbo ya Marikana ya madini ya Platinum. Watu thelathini na wanne waliuawa na polisi kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya wachimba mgodi huo wakidai malipo zaidi, wiki moja iliyopita.

Misa hiyo ilivurugwa kwa muda kufuatia kuwasili kwa mamia ya wafanyakazi wa mgodi walio katika mgomo, baadhi yao wakiwa wamebeba mapanga. Misa kama hiyo zinafanyika nchini kote Afrika Kusini.

Rais Jacob Zuma anatarajiwa kuanisha hadidu za rejea kwa tume ya kuchunguza mauaji hayo. Bwana Zuma hakushangiliwa wakati alipotembelea eneo la tukio la mgodi wa Marikana Jumatano. Mgogoro huo umesambaa katika migodi mingine ya platinum nchini humo.

Afrika Kusini inazalisha robo tatu ya madini hayo ya Platinum kote duniani na bei ya madini hayo imepanda kutokana na wasiwasi wa kushuka kwa uzalishaji nchini Afrika Kusini.