CCM Kukomesha Rushwa Wakati Wa Chaguzi
By Maganga Media - May 16, 2012
TAMKO LA NEC KUHUSU KUKOMESHA TATIZO LA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI NDANI YA CHAMA
Kikao cha NEC baada ya kujadili kwa kina changamoto zinazokikabili Chama Cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi wa ndani ya Chama kimebaini tishio la tatizo la rushwa. Hivyo NEC imesisitiza kusimamia kwa ukamilifu ahadi ya Mwanachama wa CCM inayosema;
“Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”,
Na pia kusimamia kwa nguvu zaidi Kanuni za Chama za Uchaguzi Na.33(2) inayosema:-
"Ni mwiko kwa kiongozi mgombea au mwana-CCM kutoa au kupokea rushwa. Kwa ajili hiyo, Kiongozi, mgombea yeyote wakati wa uchaguzi akithibitika kuwa ametumia rushwa katika jitihada zake za kuwania nafasi anayoiomba hatateuliwa kugombea nafasi hiyo.
Hali kadhalika, mgombea yeyote atakayethibitika kuwa ameshinda uchaguzi kwa njia ya kutoa rushwa, atanyang’anywa ushindi alioupata, na pia atazuiwa asigombee tena katika uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; au atapewa adhabu kubwa zaidi ya hiyo kama itakavyoonekana inafaa."
Hivyo basi NEC imetoa maagizo yafuatayo:-
(a) Kuanzia sasa ni marufuku kwa mgombea wa ngazi yoyote kuzunguka matawini, kwenye kata, wilayani na mikoani kukutana na Wajumbe wa mkutano utakaomchagua kwa kisingizio cha kuwasalimu Wajumbe,kuwapa nauli au kujitambulisha. Mgombea atakayethibitika anazunguka/ amezunguka ataondolewa bila kuchelewa katika orodha ya wagombea.
(b) Kwa watendaji na viongozi wa Chama wa ngazi zote kuanzia sasa ni marufuku kuwatembeza wagombea ndani ya maeneo yao kwa nia ya kuwatambulisha kwa wapiga kura. Mtendaji/kiongozi atakayebainika anakiuka agizo hili atachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja.
(c) Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji na viongozi wa Chama wa ngazi zote kuwaitia wagombea Wajumbe wa mikutano ya Uchaguzi kwa lengo lolote lile, kwani vikao vya aina hiyo havimo katika Katiba, na ni vikao haramu vinavyopalilia rushwa.
NEC imetoa wito kwa wana-CCM popote walipo wapige vita rushwa na watoe taarifa ya vitendo vya rushwa katika Ofisi za Chama na TAKUKURU. Kila mwana-CCM wa dhati awe askari wa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya adui rushwa kama ilivyo imani ya mwana CCM.
UCHAGUZI BILA RUSHWA UNAWEZEKANA, KILA MWANACHAMA, TIMIZA WAJIBU WAKO.!
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
15/05/2012
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII