HABARI MPYA LEO  

Sakata la umri wa Lulu latua Mahakama kuu

By Maganga Media - May 16, 2012

MAWAKILI wanaomtetea mwigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji, wamewasilisha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam maombi ya uchunguzi wa umri wa mteja wao. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa kutenda kosa hilo nyumbani kwa marehemu April 7, mwaka huu.
Mawakili hao waliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 7, mwaka huu wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa mteja wao ni mtoto.

Jana, mawakili wanaomtetea msanii huyo waliwasilisha maombi Mahakama Kuu wakiiomba itoe uamuzi kama Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo kwa kuwa wanaamini kuwa ina mamlaka hayo. Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka 2012, yaliyosilishwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba ya jopo la mawakili hao, pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Akifafanua juu ya maombi hayo, Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa. Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  kuifanya ijiridhishe kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kuangalia maslahi ya mtoto.

“Baada ya uchunguzi huo, mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto, basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mtoto,” alisema. Alisema kifungu hicho huelezea ulinzi na maslahi ya mtoto katika uendeshaji wa kesi kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Mawakili hao wakiwa katika Mahakama ya Kisutu, walidai kwamba msanii huyo ana umri wa miaka 17 na kwa maana hiyo bado ni mtoto na kesi yake haipaswi kusikilizwa katika mahakama za kawaida kama mtu mzima. Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo alisema bado iko kwenye upelelezi na kwamba kulingana na jinsi ilivyo isingekuwa busara kuamua hoja yoyote na aliutaka upande wa utetezi uwasilishe maombi hayo kupitia Mahakama Kuu.

Mawalili wanaomtetea Lulu ni Kibatala, Fungamtama, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo  na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 21 mwaka huu na msanii huyo bado anaendelea kusota rumande kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII