HABARI MPYA LEO  

Sajuki ainuka Kitandani!

By Maganga Media - May 29, 2012

HEBU mwacheni Mungu aitwe Mungu! Hatimaye habari njema kutoka katika Hospitali ya Saifee iliyopo jijini Mumbai, India anakotibiwa staa wa filamu za Kibongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ zinatia faraja kwa Watanzania.


Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ akiwa hospitalini nchini India.
Sajuki akiwa amepumzika, pembeni ni mkewe Wastara Juma.
 
ANYANYUKA KITANDANI, AONGEA
Habari hizo njema zinaeleza kuwa Sajuki aliyeambatana na mkewe, Wastara Juma na kaka yake, hatimaye ameweza kunyanyuka kitandani na kuongea tofauti na siku aliyoondoka Bongo na mwanzoni alipofikishwa hospitalini hapo. Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita kwa njia ya simu, Wastara alisema Sajuki alikuwa amepata nafuu na hali siyo mbaya kwani alikuwa na uwezo wa kuzungumza hivyo akampa simu ili azungumzie afya yake yeye mwenyewe jinsi anavyojisikia.

SAJUKI LAIVU
Sajuki alipopewa simu alianza kwa kuwashukuru wale wote wanaomuombea dua na kujitolea kwa hali na mali ili kuokoa uhai wake. “Namshukuru sana Mungu naendelea vizuri. Nilichukuliwa vipimo na nikabainika kuwa na uvimbe mwingi sehemu mbalimbali tumboni.

“Madaktari walibaini kuwepo kwa uchafu kwenye mapafu. Mwanzoni waligundua nina tatizo la kupumua na kukaukiwa damu. “Wamelishughulikia hilo kwanza na hapa nilipo nimezungukwa na madawa, kwa kweli najisikia nafuu,” alisema Sajuki kwa sauti ya kukwaruza.

MADAKTARI
Sajuki alisema alipokelewa vizuri lakini kabla ya kuanza matibabu ya uvimbe tumboni, madaktari walilazimika kumtibu kwanza tatizo la damu na pumzi hivyo matibabu ya kilichompeleka hospitalini hapo (uvimbe) yakawekwa pembeni.

WASTARA ATIA NENO
Kwa upande wake, Wastara alisema kuwa Sajuki alipaswa kupatiwa matibabu kwa wiki mbili ndipo warejee nyumbani lakini kwa hali halisi inaonekana watakaa zaidi kwani tayari wiki mbili zimekatika.

MATIBABU YAANZA
Wastara alisema kuwa baada ya kumalizika kwa tatizo la pumzi na kupungukiwa damu, madaktari wameanza vipimo vya tatizo la uvimbe na kusisitiza kuwa uzi ni uleule wa kumwombea mumewe ili arejee katika siha njema.

TUMEFIKAJE HAPA?
Sajuki alianza kusumbuliwa na uvimbe mwaka jana ulioanzia mkononi na baadaye ndani ya mwili kwenye ini na sasa madaktari wanasema siyo kwenye ini tu bali na sehemu nyingine tofauti za tumboni

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII