Viongozi watatu wa Chadema Tarime mbaroni kwa uchochezi!
By Maganga Media - Jun 7, 2012
VIONGOZI wa Chadema wilayani Tarime wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kuchochea ndugu wasimchukue marehemu wao kutoka mochari ya hospitali ya wilaya.
Wanaoshikiliwa ili kuhojiwa ni Mwenyekiti wa Chama wa Wilaya, Lucas Ng'oto, Katibu wa Wilaya, Marwa Mroni na Diwani wa Sabasaba, Christopher Chomete. Wanashukiwa hao wanadaiwa kushawishi ndugu wa Mgosi Magasi aliyeuawa na polisi kwa risasi waliokwenda kumkamata akidaiwa kujeruhi mlinzi wa mgodi wa North Mara, Winceslaus Petro kwa panga walipovamia mgodi huo.
Polisi imesema ushawishi huo ulisababisha uvunjifu wa amani katika maeneo ya hospitali. Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Sebastian Zakaria aliwaambia waandishi wa habari jana, kwamba wanasiasa hao walishawishi ndugu wa Magasi wasichukue mwili wake wakishinikiza kupewa maelezo ya jinsi polisi walivyomuua.
Magasi, ambaye alikuwa mkazi wa kijiji cha Nkende, aliuawa hivi karibuni kwa kupigwa risasi tumboni na polisi waliokwenda kumkamata baada ya kujeruhi kwa kumkata panga mlinzi wa mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo na unaomilikiwa na kampuni ya Africa Barrick Gold. Kwa mujibu wa Polisi, Magasi alipigwa risasi baada ya kukaidi amri ya kukamatwa. Petro anapata matibabu ya majeraha katika Hospitali ya KCMC Moshi.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII