HABARI MPYA LEO  

Kamati kuchunguza kiwanja kilichomng'oa Mkulo

By Maganga Media - Jun 7, 2012


KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeunda tume ndogo kuchunguza uuzwaji wa Kiwanja Namba 10 ambacho kilikuwa kinamilikiwa na Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), kabla ya kuuzwa katika mazingira tata kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL).

Kiwanja hicho ni miongoni mwa sababu zilizomng’oa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuonyesha jinsi alivyoshiriki kwa namna moja au nyingine katika uuzaji wa kiwanja hicho huku akiivunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe alisema kutokana na mgogoro wa uuzaji wa kiwanja hicho, wamepokea ripoti maalumu kutoka CHC ambayo imeonyesha uuzaji wa kiwanja hicho pamoja na mali za Serikali zilizokuwa zinamilikiwa na NMC.

Sakata la Kiwanja namba 10 kilichouzwa MeTL, lilianza kunukia Oktoba 10 mwaka jana, baada ya Mkulo kuamua kuvunja ghafla bodi ya CHC kabla haijamaliza muda wake mnamo Desemba 31. Awali, bodi hiyo ilikuwa imalize muda wake Juni 30, 2011, lakini Mkulo alitumia mamlaka yake kuongeza muda hadi Desemba 31. Hata hivyo, ghafla alibadili uamuzi huo wakati bodi hiyo ilipaswa kupokea ripoti ya uchunguzi wa kiwanja hicho

Zitto alisema kutokana na utata huo huku mali za NMC zikiwa hazijulikani vema, kamati yake imeunda tume ndogo kuchunguza suala hilo, ili waweze kuwasilisha taarifa bungeni na kutoa uamuzi na kuishauri Serikali kuhusu suala hilo.

“Suala la uuzaji wa Kiwanja Namba 10 ni nyeti sana, yaani bado ngoma nzito. Linahitaji umakini wa hali ya juu ili kulimaliza. Kutokana na hali hiyo, tumeamua kuunda kamati ndogo ambayo itafanya uchunguzi na kutoa taarifa bungeni ili tuweze kuchukua hatua,” alisema Zitto.
Alisema mpaka sasa, NMC bado iko hai, ina mkurugenzi ambaye analipwa mshahara kutokana na pango la majengo yake, lakini cha kushangaza hawana kitabu cha benki kinachoonyesha kiasi cha fedha zilizopo ambazo zimetokana na pango hilo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangwala, amesusa kujadili bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutokana na vitabu kuchelewa kuwafikia wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii.

Baada ya Dk Kigwangwala kususa kushiriki, wabunge wengine walimsihi kuendelea ili aongeze nguvu ya wabunge waliokuwa hawaridhishwi na bajeti hiyo, lakini alishikilia msimamo wake. Mbunge huyo alisema ataendeleza hatua yake hiyo kwenye kikao cha muhtasari Jumatatu mjini Dodoma. “Nimesusa na kumtaka katibu wa kamati aingize kwenye kumbukumbu rasmi kuwa nimerudisha vitabu na sitajadili mpaka tutakapopewa muda wa kutosha wa kusoma kwanza na kuchambua na siyo kulipua lipua tu,”

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII