HABARI MPYA LEO  

Wahisani kusaidia bajeti 2012/13

By Maganga Media - May 11, 2012

 
WASHIRIKA wa Maendeleo nchini wametangaza kuingiza Sh bilioni 776 katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha ujao, huku wakieleza kufurahishwa na jinsi taasisi za kusimamia Serikali ikiwamo Bunge, Kamati zake na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinavyofanya kazi zao.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Umoja wa Ulaya (EU), washirika hao wa maendeleo kupitia Mfuko Mkuu wa Bajeti (GBS), wameahidi kutoa zaidi ya nusu ya fedha hizo katika robo ya kwanza ya mwaka huo wa fedha, ili kurahisisha utekelezaji wa Bajeti hiyo ya Serikali.

Taarifa hiyo ya EU ilieleza, kwamba fedha hizo ambazo ni dola milioni 495 ni mchango mkubwa wa washirika hao wa maendeleo katika kuunga mkono utekelezaji wa mpango wa kupunguza umasikini na wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Washirika wa maendeleo wanaochangia GBS ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Canada, Denmark, EU, Finland, Ujerumani, Ireland, Japan, Norway, Sweden, Uingereza na Benki ya Dunia. EU imekuwa Mwenyekiti wa kundi hilo kwa miezi 12 iliyopita na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DID) sasa litachukua jukumu hilo. Itaanza uenyekiti mwezi huu.

Washirika hao wamesema wametoa fedha hizo kutokana na mambo makuu matatu; kuridhishwa na mapitio ya mwaka ya 2011; kuimarika kwa mazungumzo katika baadhi ya sekta muhimu mwaka uliopita na mabadiliko ya GBS kwa miaka miwili iliyopita yaliyosaidia ufuatiliaji kwa miaka kadhaa, wa jinsi fedha za umma zinavyotumika.

“Matukio ya hivi karibuni yameonesha kwamba taasisi za kuisimamia Serikali nchini zinatimiza majukumu yake katika kufanya tathmini ya ufanisi wa Serikali na kutaka hatua zichukuliwe pale ambapo pameonekana kuwa na udhaifu,” ilieleza taarifa hiyo ya EU.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII