HABARI MPYA LEO  

Arsenal na Ligi ya Mabingwa Ulaya

By Maganga Media - May 13, 2012

Ferguson
Moja ya mambo yanayotafutwa kwenye mbio za Ligi Kuu ya Uingereza ni nafasi za timu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.Kwa minajili ya Uingereza wakati huu, panaweza kuwapo nafasi moja au mbili, wakati timu zinazowania ni Arsenal wenye pointi 67,
Tottenham waliojikusantia pointi 66 na Newcastle waliovuna pointi 65.

Mechi muhimu katika kuamua hili ni kati ya Everton na Newcastle; Tottenham Hotspur dhidi ya Fulham na West Brom wanaoikaribisha Arsenal. Hali ilivyo ni kwamba hatima ya Arsenal imo mikononi mwao wenyewe, kwa maana kwamba wanachotakiwa ni kushinda tu ili kufuzu moja kwa moja, bila kusubiri matokeo ya mechi nyingine. Ushindi utawahakikishia kubaki nafasi ya tatu wanayoshikilia

Hata hivyo, ikiwa Arsenal watatoa sare dhidi ya Baggies, wanaweza kuvukwa na kutupwa nafasi ya nne ikiwa Tottenham watawafunga Fulham. 

Maana yake ni kwamba Washika Bunduki hao wa London hawatakuwa na chaguo zaidi ya kuingia kwenye mechi za mchujo ili kufuzu, huku Spurs wakisonga moja kwa moja kwenye mashindano hayo makubwa ya Ulaya.

Ikiwa Arsenal watachezea kichapo nyumbani kwa West Brom, ni dhahiri pia watakuwa wamejiweka pabaya, kwa sababu wataweza kupitwa na Spurs watakaohitaji sare tu ikiwa Arsenal itafungwa mabao mawili au zaidi. Arsenal pia watapitwa na Newcastle inayonolewa na Alan Pardew, ikiwa watawafunga Everton.

Vinginevyo ni kwamba Tottenham wakishinda mechi yake tu itakuwa imejihakikishia kupata nafasi ya nne na sare pia inaweza kuitosheleza ikiwa Newcastle hawatawafunga Everton.

Kwa upande mwingine, ili Newcastle waweze kuingia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lazima wawafunge Everton na kuomba ama Arsenal au Tottenham wasishinde mechi zao. Ikiwa hizo tatu zitatokea, basi Newcastle itamaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, ikiwa Chelsea itatwaa Kombe la Mabingwa Ulaya kwenye fainali dhidi ya Bayern Munich mjini Munich Mei 19 mambo yatabadilika Uingereza, kwa sababu timu itakayoshika nafasi ya nne kwenye EPL mwaka huu haitakuwa na nafasi kwenye ligi hiyo tena.

Badala yake, timu hiyo itaingia kwenye Ligi ya Europa pamoja na watakaomaliza ligi wakiwa nafasi ya tano, kwani timu inayotwaa kombe hilo inashiriki msimu unaofuata kulitetea.

Katika mazingira haya, Arsenal watatakiwa kutumia vyema nguvu na fursa kuwamaliza West Brom, kwani kwao msimu ni kama umeshaisha tu, hawana kikubwa cha kupata wala kupoteza.

Spurs wanaelekea pia kwamba watawafunga Fulham, na maana ya haya ni kwamba kuna kila dalili za Newcastle kuachiwa simanzi bila kupenda.

Pengine Bayern watalitwaa kombe la Ligi ya Mabingwa, na kwa kufanya hivyo mazingira ya Ligi kuu ya England na ushiriki wa msimu ujao kimataifa kutoathiriwa.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII