HABARI MPYA LEO  

Waasi wa Syria wakataa kusaini makubaliano zaidi

By Maganga Media - Apr 10, 2012

Waasi nchini Syria

Mpango wa amani wa Syria unaelekea kuwa hatarini baada ya kiongozi wa waasi, Kanali Riyadh al-Asaad, kukataa masharti mapya ya serikali ya Syria yanayowataka waasi hao kuwaondoa wapiganaji wao katika maeneo ya mapigano.

Mpango wa kuleta amani nchini Syria ulioandaliwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, unaitaka serikali ya Syria pamoja na waasi kuondoa wanajeshi katika maeneo ya mapigano ifikapo kesho. Mapigano yote yanapswa kusitishwa kabisa masaa 48 baadaye. Lakini utawala wa Syria umeeleza kwamba utaufuata mpango huo iwapo waasi watasaini mkataba unaohakikisha kwamba watasitisha mapigano.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan
Hata hivyo, matakwa hayo yamekataliwa na Kanali Riyadh al-Asaad, ambaye ni kiongozi wa waasi. Riyadh aliliambia shirika la habari la AFP kwamba yeye pamoja na wanajeshi wake wako tayari kuufuata mpango wa amani wa Kofi Annan na kwamba watatoa ahadi ya kufanya hivyo kwa jumuiya ya kimataifa lakini si kwa utawala wa Syria. Uongozi wa Syria umezitaka pia serikali za Qatar, Saudi Arabia, na Uturuki kuwasilisha ahadi ya maandishi ya kutokuwafadhili waasi.

Baba Mtakatifu ataka amani irejee Syria
Tamko la waasi linakuja baada ya siku mbili za mapigano yaliyosababisha vifo vya Wasyria wapatao 180. Katika mahubiri yake ya Sikukuu ya Pasaka, Papa Benedikt wa 16 alizungumza juu ya amani na kugusia hasa hali nchini Syria. "Mapigano yanapaswa kumalizika, hasa nchini Syria," alisema Baba Mtakatifu. "Njia ya kuheshimiana, ya mazungumzo na ya maridhiano ndio inayotakiwa kufuatwa. Jambo hilo linaendana pia na matakwa ya Jumuiya ya Kimataifa."

Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 katika ibada ya Pasaka
Wakati huo huo, China imeitaka Syria kuheshimu mpango wa amani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Liu Weimin, amezitaka pande mbili zinazopigana kuacha mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa mwaka mmoja sasa. Waziri huyo ameitaka pia Jumuiya ya Kimataifa kuwa na subira na kumpa Kofi Annan muda zaidi.

Hapo kesho, Kofi Annan atafanya ziara nchini Uturuki na kutemebelea kambi ya wakimbizi kutoka Syria. Afisa mmoja wa ubalozi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ziara ya Annan itachukua muda wa masaa machache tu. Jumatano, Annan anatarajiwa kuitembelea Iran. Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Walid Muallem, leo atawasili nchini Urusi ambapo kesho atakutana na waziri mwenzake wa nchi hiyo, Sergei Lavrov.

DW

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII