HABARI MPYA LEO  

Rais Toure ajiuzulu kwa masharti

By Maganga Media - Apr 10, 2012

Waziri wa Nje wa Mali Dioncounda na Spika wa Mali Traore



Rais Amadou Toumani Toure wa Mali amekubali rasmi kujiuzulu kwa makubaliano na viongozi wa mapinduzi kumaliza mgogoro unaolitafuna Taifa hilo la Magharibi. Mpatanishi wa Kimataifa Djibril Bassole, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, amethibitisha kuwa barua ya kujiuzulu imewasilishwa. Kujiuzulu huko kunafungua njia kwa viongozi wa mapinduzi kukaa pembeni na kumwachia spika wa Bunge kuchukua nafasi.
Mali imekuwa ikipambana na kundi lililojitenga kaskazini mwa nchi. Limeongezeka nguvu baada ya mapinduzi yaliyofanywa na maafisa wa jeshi Machi 22.

Vikwazo vyaondolewa

Bw Bassole, anayewakilisha Muungano wa nchi za Magharibi kiuchumi wa ECOWAS alikutana na Bw Toure katika mji mkuu wa Mali,Bamako. "Ndio tumepokea tu barua rasmi ya kujiuzulu kutoka kwa Rais Amadou Toumani Toure," aliwaambia waandishi wa habari. "Sasa tutawasiliana na mamlaka zinazotakiwa ili nafasi ya Rais ithibitishwe na ili kwamba tuweze kuchukua hatua zinazostahiki."

Chini ya makubaliano hayo, Spika wa Bunge la Mali Dioncounda Traore, atachukua nafasi ya Urais kwa muda na kuongoza utawala wa mpito mpaka uchaguzi utakapofanyika. Akishaapishwa, Bw Traore ana siku 40 kuandaa uchaguzi, makubaliano hayo yanaeleza. Bw Traore, ambaye amekuwa Burkina Faso tangu mapinduzi yatokee alisema anaondoka kuelekea Bamako: "Ninaondoka kuelekea Mali na moyo wangu ukiwa na matumaini makubwa.”

"Nchi yangi imepitia magumu mengi lakini ninaondoka nikiwa na matumaini watu wa Mali wataungana kupambana na hali hii kwa ujasiri."

Ecowas imeondoa vikwazo ilivyoviweka baada ya mapinduzi na imekubali msamaha utolewe kwa viongozi wa mapinduzi. Mapinduzi hayo yaliyoongozwa na Kepteni Amadou Sanogo, yalitokea wakati kukiwa na tuhuma kutoka kwa jeshi la nchi hiyo kuwa serikali ilikuwa haijishughulishi vya kutosha kupambana na waasi kaskazini mwa nchi.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII