KILI Music Awards yataja viingilio
By Maganga Media - Apr 6, 2012
VIINGILIO kwa ajili ya hafla ya utoaji wa Tuzo za Muziki Tanzania itakayofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam Aprili 14, mwaka huu vimetangazwa, ambapo cha juu ni sh 75,000 huku cha chini kikiwa ni sh 20,000. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, ambao ndio wadhamini wa tuzo hizo, George Kavishe, alisema kiingilio cha sh 75,000 ni maalumu kwa siti maalumu, ambapo pia kutakuwa na chakula cha usiku, vinywaji bia na mvinyo, huku siti za kawaida ni sh 20,000 na bia ya Kilimanjaro.
Kavishe alisema usiku huo wa utoaji tuzo kwa wasanii, utasindikizwa na wasanii wa nyumbani, ambao ni Diamond, kundi la TMK Wanaume, Charles Baba, Khalid Chokoraa, Recho, Ommy Dimples na Hassan Bichuka. “Tumevuka lengo la idadi ya kura kwa nyanja zote, ikiwa ni maana ya ujumbe mfupi, vipeperushi, barua pepe na mitandao, hii inamaanisha tuzo zimekubalika na zimepokewa vizuri,” alisema.
Pia Kavishe amelishukuru Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa bia ya Kilimanjaro na kuipa tena kibali cha kudhamini na kuendesha shughuli za Tuzo za Muziki Tanzania.
Tiketi hizo zitauzwa kuanzia Jumatatu ijayo, Mlimani City, Baraka Garden Posta, Mtaa wa Azikiwe, Zizzou Fashion ya Victoria, Sinza na Tegeta, Born to Shine Mwenge, Robbie One Fashion Kinondoni na Engine Petrol Station Mbezi.
Aidha, Kavishe alitoa shukrani kwa Watanzania, kujitokeza kwa wingi katika zoezi la kuwapigia kura wasanii wanaotaka washinde tuzo hizo.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII