HABARI MPYA LEO  

ZITTO KUGOMBEA URAIS 2015

By Maganga Media - Mar 25, 2012

Zitto Kabwe, Naibu katibu mkuu CHADEMA
 
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Zitto Kabwe ameibuka na kusema kuwa anataka kuwa rais wa Tanzania mwaka 2015.Wakati Zitto akitoa kauli hiyo nzito, Waziri  wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta naye amesema anashangazwa na watu wanaoweweseka wanaposikia kuwa mwanasiasa huyo anayeongoza vita dhidi ya ufisadi ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, anataka kuwania urais.

Kauli hiyo ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni huenda ikaibua mjadala mzito ndani ya chama chake, ukiacha zile mbio za vigogo wa CCM wanaotajwa kuutaka urais 2015. 

Katika taarifa yake aliyoituma jana kwa gazeti la Mwananchi Jumapili, Zitto alisema; “ Kwanza niseme wazi kabisa kuwa Urais ninautaka, nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto hizi. Ninaamini ninaweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kukabili changamoto hizi.”  Alitamba anao uwezo kwa kuwa ni mzalendo, mwenye utashi wa kuleta mabadiliko stahiki kulingana na nchi inavyoongozwa.   Katika taarifa hiyo ameeleza kuwa kwa sasa nchi imesahau maendeleo ya watu badala yake imejikita katika maendeleo ya vitu.

 “Ninajua kuwa hivi sasa viongozi wetu wengi wanaangalia zaidi mitindo badala ya mambo ya msingi,” Zitto amesema taarifa na kuongeza:   “Ninajua kuwa maendeleo vijijini yamesahaulika, ninajua nchi yetu inahitaji uongozi wa kufanya mabadiliko makubwa badala ya mabadiliko ya juujuu.”  Alieleza kuwa mabadiliko makubwa  yanahitaji  maamuzi magumu yatakayoudhi wengi hasa vigogo wa nchi za Magharibi huku akitoa mfano kuwa ni pamoja na kuzuia nchi kuuza malighafi pekee.   Alisisitiza kuwa rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo ya nchi na kwamba lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuzuia na kutokomeza ufisadi.  

“Rasilimali kama madini, mafuta, gesi asilia, ardhi na nyinginezo ni lazima zifaidishe wananchi wa nchi yetu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.  Sababu za kutaka  Urais  Katika taarifa hiyo Zitto alieleza kuwa kwa sasa nchi inahitaji kiongozi wa juu atakayekabili changamoto muhimu na kwamba yeye anaweza kuwaongoza Watanzania kukabiliana na changamoto hizo.  “Sio kazi rahisi, lakini ni kazi ambayo lazima Mtanzania mmoja aifanye, mimi nataka kuifanya, nina uwezo wa kuifanya,” alitamba katika taarifa hiyo.
 

Samwel Sitta 
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amevunja ukimya na kutema cheche kuhusu suala la kugombea urais katika uchaguzi wa 2015 na kusema kuwa wanaomkataza kuzungumzia suala hilo wameingiwa kiwewe.Sitta ambaye amekuwa akitajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo, amesema itakapofika wakati wa kutangaza nia yake hakuna mtu atakayemzuia.

Alisema hayo wakati akifungua Bonanza la Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, lililofanyika Msasani Beach. "Linapoingia suala la Urais kuna watu wanapata kiwewe, wanaposikia ninataka kugombea, lakini hiyo ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa anaruhusiwa kugombea," alisema Sitta. Alisema muda utakapowadia wa yeye kufanya hivyo, hakuna atakayemzuia kugombea nafasi hiyo kwa sababu atakuwa anatumia haki yake kikatiba.

Alisema kuna baadhi ya watu wanatumia vibaya maneno ya Rais Jakaya Kikwete kwa kueleza kiongozi atakayemfuata lazima awe kijana, kitu ambacho Sitta alisema kamwe Rais hakumaanisha hivyo. Alisema Watanzania wamechoshwa kila siku kusikia habari za rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma na kusababisha gharama za ujenzi wa miradi mbalimbali kuwa juu kwa manufaa ya watu wachache.

Maganga Media

 CHANZO: Gazeti la MWANANCHI

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII