HABARI MPYA LEO  

MTIKILA KIZIMBANI

By Maganga Media - Mar 14, 2012

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila ana kesi ya kujibu katika kesi ya kuchapisha na kuusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi baada ya kuwaleta mahakamani hapo mashahidi watano.
Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa serikali, amebaini kuwa Mchungaji Mtikila ana kesi ya kujibu na kwa maana hiyo mchungaji huyo maarufu kwa kukabiliana na kesi za uchochezi, atatakiwa kupanda kizimbani Aprili 11 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kujitetea.
Baada ya uamuzi huo, Mtikila ambaye hana wakili wa kumtetea na kuamua kujitetea mwenyewe, alidai kuwa anatarajia kuleta mashahidi 10 wa kumtetea katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini.
Februari mwaka huu, Mtikila alikiri maelezo aliyochukuliwa na ofisa wa polisi kuwa ni yake na kwamba hana pingamizi nayo, hivyo mahakama iliyapokea kama kielezo cha upande wa mashitaka.

Mtikila katika maelezo hayo, alikiri kuwa kweli aliuandaa waraka huo na kuusambaza, lakini alikanusha kwamba haukuwa wa uchochezi kwani unahusu maneno ya Mungu.
Mtikila alikiri maelezo hayo yaliyosomwa na kutolewa mahakamani kama kielelezo baada ya shahidi wa Serikali, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Ibeleze Mrema (54), kudai kuwa Aprili 15, mwaka 2010 akiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam, aliitwa na mkuu wake wa kazi na kumpa kazi ya kumhoji Mtikila kuhusu tuhuma za kukutwa na waraka wa uchochezi.
Alidai kuwa wakati akimhoji mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na nyaraka hizo na kwamba alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya kuokoa Wakristo na aliusaini yeye Mtikila waraka huo.
“Mtikila alikiri kuhusika kuandaa waraka huo kama mwenyekiti, aliusaini kwa niaba ya wengine … nilipomhoji walichapisha wapi Mtikila hakupenda kusema bali alidai kuwa zilikuwa nakala 100,000 ambazo zilisema kwamba Rais Kikwete anaangamiza Ukristo na amekuwa jasiri kuingiza Uislamu katika Katiba ya Jamhuri,” alidai Mrema.
Mrema aliendelea kudai kupitia maelezo hayo kwamba, Mtikila alikuwa anahamasisha Wakristo wajitoe mhanga kukomesha ugaidi na wamuweke rais Mkristo Ikulu.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshitakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema ‘Kikwete kuuangamiza Ukristo', ‘Wwakristo waungane kuweka mtu Ikulu’ alinukuliwa Mtikila.
Katika shitaka la pili, Aprili 16, mwaka 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii.

http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII