HABARI MPYA LEO  

Dunia yalaani mapinduzi Mali

By Maganga Media - Mar 23, 2012


Baada ya jeshi la Mali kutangaza kuipindua serikali ya rais Amadou Toumani Toure, kumekuwa na shutma za kimataifa dhidi ya wanajeshi hao. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limetaka utawala wa kikatiba kurejeshwa nchini humo, huku Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo barani Afrika wakisema wanasitisha baadhi ya shughuli nchini humo.

Msemaji wa wanajeshi waasi nchini Mali amesema jeshi litarejesha demokrasia nchini humo na kuwa umoja utarejea hivi karibuni. Kufikia sasa haijulikani alipo Rais Amadou Toumani Toure, lakini taarifa ya televisheni ya taifa ilisema kuwa rais huyo yuko katika hali nzuri ya kiafya.

Sababu kuu ya wanajeshi hao kuasi na hatimaye kuchukuwa madaraka ya nchi, ni kile walichokiona kama ulegevu wa serikali katika suala la vita dhidi ya waasi wa Toureg, kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa kipindi sasa, wanajeshi walikuwa wakilalamikia upungufu wa vifaa vinavyotolewa na serikali kupambana na waasi hao, ambapo mapigano makali katika miezi ya hivi karibuni yamegharimu maisha ya watu kadhaa na kuwalazimisha takribani raia 200,000 kuzikimbia nyumba zao.

Mwezi uliopita mamia ya watu waliandamana katika mji mkuu, Bamako, kuilalamikia serikali kushindwa kuwadhibiti waasi wa Toureg, ambao wengi wao wana silaha kutoka serikali ya zamani ya Libya, chini ya Marehemu Muammar Gaddafi.


Maganga Media

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII