HABARI MPYA LEO  

Vielelezo umri wa Lulu vyawasilishwa mahakama kuu

By Emmanuel Maganga - Jun 16, 2012

Mawakili wa utetezi katika kesi ya mauaji ya Steven Kanumba (28) inayomkabili msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael (18) maarufu Lulu, wamewasilisha Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam vielelezo vya kuthibitisha kwamba mteja wao ana umri wa miaka 17.

Vielelezo hivyo, viliwasilishwa jana mahakamani hapo kwa njia ya maandishi kupitia kiapo na jopo la mawakili hao mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaib anayechunguza umri halali wa mshtakiwa huyo.

Katika ushahidi uliowasilishwa, baba mzazi wa Lulu, Michael Kimemeta, ameapa kwamba binti yake hadi anatuhumiwa kufanya tendo hilo la mauaji umri wake ni miaka 17.

Kimemeta anadai kwamba, Lulu alizaliwa miaka 17 iliyopita akiwa mkoani Kilimanjaro.

“Wakati anazaliwa binti yangu nilipata taarifa nikampa jina la Elizabeth Michael wakati huo mama yake Lucresia Kalugila alikuwa tayari kampa jina la Diana Michael” alisema na kufafanua:

“Baada ya kumfahamisha napenda aitwe Elizabeth ililazimika kuongeza Diana Elizabeth Michael Kimemeta, majina yote mawili ni yake.”

Alidai kuwa, Lulu alibatizwa Septemba 28, mwaka 1997 katika Kanisa Katoliki la Chang’ombe na ushahidi wa cheti cha ubatizo upo.

Kwa upande wake, Kalugila ambaye ni mama mzazi wa Lulu, alidai kuwa alijifungua mtoto huyo miaka 17 iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ya Jijini Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri unaoongozwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimario, utajibu ushahidi huo Juni 20, mwaka huu na maombi hayo yatasikilizwa Juni 25 mwaka huu.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII