HABARI MPYA LEO  

Uamuzi wa mahakama Misri walaumiwa.

By Unknown - Jun 16, 2012

Mahakama kuu ya katiba nchini Misri imesababisha hali ya wasiwasi nchini humo baada ya kutangaza kuwa uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwaka jana ulikuwa kinyume cha katiba na kutaka ufanyike upya.

Maandamano Misri

Uamuzi huo wa mahakama uliotolewa siku mbili kabla ya kufanyika duru ya pili ya kinyang'anyiro cha urais, unalipa baraza la utawala wa kijeshi nguvu za bunge. Wanaharakati na wanasiasa wamelishutumu jeshi kwa kufanya mapinduzi.

Kulingana na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, uamuzi huo una athari kubwa hasa kwa kuwa umetolewa kabla ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi mwishoni mwa juma, na inamaanisha sasa kwamba mamlaka ya bunge nchini humo yamo chini ya baraza kuu la Kijeshi ambalo lilipewa jukumu la kuongoza Misri katika kipindi cha mpito baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak kung'olewa madarakani.

Pia kwa msingi wa uamuzi huo, Misri haina katiba kwa sasa na haina bunge.

Chama cha Muslim Brotherhood tayari kimeelezea hofu yake kuwa hatua chache ambazo nchi hiyo ilikuwa imepiga kidemokrasia zinazidi kutoweka.

Chama hicho kimeonya kuwa huenda kukazuka vurumai nchini humo hasa iwapo madaraka ya nchi hiyo yatakabidhiwa kwa watu walio na uhusiano na serikali iliopita ya Hosni Mubarak.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII