Ugiriki yapata kiongozi mpya
By Unknown - Jun 18, 2012
Kiongozi wa chama cha New Democracy nchini Ugiriki, chenye sera za mrengo wa kulia, Antonis Samaras, ameshinda katika uchaguzi mkuu wa pili ambao umefanyika wiki sita baada ya ule wa kwanza.
Bwana Samaras amesema wananchi wa Ugiriki wameeleza nia yao ya kutaka kubakia katika muungano wa nchi za Ulaya na kuheshimu nia ya nchi hiyo katika kuimarisha uchumi wake.
Amevitaka vyama ambavyo vina malengo sawa na chama hicho kuunda serikali thabiti.
Naye Kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto cha Syriza, Alexis Tsipras, amesema chama chake hakitajiunga katika serikali ya pamoja.
Bwana Tsipras amesema chama chake bado kinapinga hatua zilizopendekezwa na nchi wanachama wa Euro kuimarisha uchumi wa Ugiriki.
Akiwahutubia wafuasi wake mjini Athens, Bwana Tsipras amesema kukiunga mkono chama cha Syriza kumezionyesha nchi za Ulaya na viongozi wa siasa wa Ugiriki kwamba hawawezi kuweka masharti ya kunusuru uchumi wa nchi hiyo bila kukubaliwa na wananchi.
Viongozi wa nchi za Ulaya walionya kuwa ikiwa raia wa Ugiriki watapinga mpango huo uliopendekezwa wa kufufua uchumi wao, basi nchi hiyo italazimika kuacha kutumia sarafu ya Euro.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble amesema matokeo ya uchaguzi huo yameonyesha nia ya raia wa nchi hiyo kuendelea na mpango wakunusuru uchumi wa nchi yao.
Mawaziri wa fedha kutoka nchi wanachama wa umoja wa ulaya, katika taarifa ya pamoja wameelezea kuwa wawakilishi wa benki kuu ya umoja huo, shirika la fedha duniani (IMF) na tume ya umoja huo watazuru nchi hiyo punde tu serikali mpya itakapoundwa.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII