HABARI MPYA LEO  

MONUC chanzo cha mgogoro DRC

By Maganga Media - Jun 13, 2012


Shirika la kimataifa la utatuzi wa migogoro (International Crisis Group, ICG ) limeonya kuwa huenda machafuko yanayoendelea mashariki wa Demokrasi ya Congo yakaongezeka. Shirika hilo limekishutumu kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa nchini humo, MONUSCO kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake kuu la kulinda raia.
Katika barua ya wazi kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, shirika la ICG linataka baraza hilo kutathmini utendakazi wa kikosi cha kutunza amani cha umoja wa mataifa MONUSCO ili kuhakikisha kwamba baadhi ya makosa ambayo yametendeka hayarudiwi tena baada ya kuongezwa kwa muda wa kikosi hicho kuendelea kuhudumu nchini Congo. Kabla ya muda huo kuongezwa shirika hilo la ICG linataka baraza la usalama la umoja wa mataifa kushinikiza serikali ya congo kumkamata mbabe wa kivita Bosco Ntaganda anayesakwa na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.

ICG, imesema usalama wa kudumu utakuwepo ikiwa kutakuwa na maelewano ya pamoja kati ya taasisi mbali mbali zinazowajibika na mzozo wa Congo.

Katika matamshi ambayo huenda yakazidisha uhasama baina ya mataifa ya Rwanda na Congo, shirika la ICG linataka baraza la usalama la Umoja wa mataifa kushinikiza serikali ya Rwanda kukoma kuunga mkono makundi ya wapiganaji yanayozua vurugu mashariki mwa Congo. Serikali ya Rwanda imekana madai kuwa inawaunga mkono wapiganaji wa waasi mashariki mwa Congo.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII