HABARI MPYA LEO  

Majibu ya Msigwa kwa Mwigulu

By Unknown - Jun 20, 2012

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amejibu pendekezo la Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba la kutaka wapinzani waombewe, akisema hakuna kanuni yoyote ya uchumi inayosema Serikali ikiendesha mambo isivyo yanafanyika maombi.

Badala yake, alisema yeye ambaye ni mchungaji huwa wanaombea wazinzi na watu waotembea na wake za watu, na si matatizo ya kiuchumi.

“Inashangaza sana kuona watu wanaunga mkono bajeti…, kila mwaka deni la taifa linaongezeka na sasa limefika Sh20 trilioni, fedha ambazo ukizigawanya kila Mtanzania atakuwa anadaiwa Sh400,000” alisema Msigwa.

“Nilivyokuwa naona wabunge wamevaa suti na wanachangia hoja bungeni nilipenda jambo hilo na kutamani siku moja niwe mbunge, lakini baada ya kuingia bungeni nimegundua kuwa hakuna kitu.”

Alisema bunge hilo hivi sasa halieleweki na kwamba mbunge mwenye elimu ya kutosha akisimama kuchangia hoja huwezi kumtofautisha na mtoto wa darasa la pili.

“Yaani mbunge profesa akisimama kuchangia hoja huwezi kumtofautisha na mtoto wa darasa la pili, watu wenye akili, akili zao wameziweka mfukoni na kuweka ushabiki wa vyama mbele, tumekuja bungeni kumaliza matatizo sio kuongeza matatizo” alisema Msigwa.

Huku akitumia mifano ya wanasaikolojia mbalimbali Msigwa alisema ni aibu kuona Watanzania wanazidi kuwa maskini harafu kila mwaka yanayozungumzwa ni tofauti na yanayotendeka.

“Ufikie wakati wabunge tutambue kuwa tumekuja hapa bungeni kuwatumikia wananchi, Watanzania waliotuchagua wanateseka na wabunge hapa bungeni mnazungumza maneno ya khanga tu,” alisema Msigwa.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII