HABARI MPYA LEO  

Ahueni kwa tasnia ya Filamu

By Unknown - Jun 20, 2012



Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akiongea na baadhi ya Viongozi wa mashirikisho ya wasanii wa filamu na Muziki kuhusu urasimishaji wa kazi za wasanii wa Filamu na Mziki jijini Dar es Salaam (jana). Serikali imeamua kuweka mfumo rasmi utakaowawezesha Wasanii wa Filamu na Muziki nchini kunufaika na kazi wanazozibuni na kuzitengeneza.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Viongozi wa Mashirikisho ya Wasanii wa Filamu na Muziki.

Dkt. Mukangara amesema kuwa Serikali imesikia kilio cha Wasanii kwa kuirasimisha Sekta ya Filamu na Muziki ili kuondokana na kilio cha muda mrefu cha Wasanii kutonufaika na jasho lao.

Amesema kuwa Serikali itatumia mfumo wa kuziwekea kazi hizo stampu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zitakuwa na usalama kwa nia ya kuondokana na uzalisha na udurufishaji ovyo wa kazi hizo na kazi hizo zitawekewa ‘bar code’ kwa wepesi wa ufuatiliaji.

Urasimisaji huu unaotarajia kuanza rasmi Januari, 2013 utawezesha wasanii kukopesheka ili kupata mitaji itakayowawezesha kutengeneza kazi bora na zenye viwango na zitakazoweza kuingia katika soko la ushindani. Ameeleza Dkt. Mukangara.

Amesema kuwa kwa sasa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Wizara ya Fedha; na Wizara ya Viwanda na Biashara zinaweka katika mfumo wa kielektroniki taratibu zinazowezesha utekelezaji wa mfumo huu kuwa rahisi.

Aidha, Dkt. Mukangara ametoa wito kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha kero ya Wasanii kuibiwa na kutofaidika na kazi zao inaondoka na kuwataka vijana kujipanga vizuri ili kuitumia fursa hii na hata katika siku za usoni waweze kuwa na Saccos za vijana katika tasnia ya filamu na muziki na waweze kukopesheka kupitia Mfuko wa Vijana.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII