HABARI MPYA LEO  

Wakili wa Lulu ateuliwa kuwa Jaji

By Unknown - Jun 20, 2012

RAIS Jakaya Kikwete amemwapisha kuwa Jaji wakili wa kujitegemea, Joaquine De-Mello ambaye alikuwa akimtetea msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) anayetuhumiwa kwa mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Wakili huyo, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King ya mwaka 2012 na ambaye alikuwa pia alikuwa mmoja wa makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) ni miongoni mwa majaji 10 walioapishwa jana na Rais Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
De-Mello ni miongoni mwa mawakili wanne waliojitokeza Aprili mwaka huu kumtetea Lulu katika kesi hiyo ya mauaji inayomtuhumu kumuua usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu.

Mawakili wengine wanaomtetea Lulu ambaye umri wake umekuwa na utata ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.

Akizungumza kwenye viwanja vya Ikulu, De-Mello alisema baada ya kuteuliwa kuwa Jaji, sasa atafanya kazi hiyo na moja ya mikakati yake ni kukabiliana na changamoto za wingi wa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Majaji wengine walioapishwa jana na Rais Kikwete ni Francis Mutungi, John Mgeta, Patricia Fikirini, Sam Rumanyika, Salvatory Bongole, Jerald Alex, Mathew Mwaim, Jacob Mwambegele na Latifa Mansook.
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema amefurahi kuteuliwa kwa majaji hao na anawafahamu kuwa wote ni wazoefu na watatekeleza kazi zao kikamilifu.

“Wote ni wazoefu. Ukiangalia utaona kuwa sita walikuwa wakifanya kazi mahakamani (Mahakama Kuu na Rufani), wawili mawakili wa kujitegemea na wawili pia mawakili wa Serikali,” alisema Jaji Othman.
Alisema majaji hao wote kabla ya kupangiwa kazi rasmi itabidi waanze kufanya kazi ya kukabiliana na kesi zaidi ya 2,200 zilizopo katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi.

Uteuzi wa majaji hao 10, alisema unaifanya Mahakama Kuu sasa kuwa nao 69 tofauti na wale 16 wanaounda Mahakama ya Rufani.
Othman alisema pamoja na uteuzi huo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kulundikana kwa kesi nyingi kuliko uwezo wao.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII