HABARI MPYA LEO  

Ananilea Nkya-Serikari Lini Itatibu Chanzo Cha Mgomo Wa Madaktari?

By Emmanuel Maganga - Jun 30, 2012

Katika nchi yeyote duniani serikali ndiyo yenye jukumu la kuweka mazingira mazuri katika hospitali za umma na kuhakikisha kuwa madaktari na wafanyakazi wa afya wanafanya kazi yao ya kutibu wagonjwa kwa furaha .

Hii ni kwa sababu serikali iliyowekwa madarakani na wananchi moja ya kazi ya kodi inayokusanya kutoka kwa wananchi ni kuhakikisha kuwa hospitali, vituo vya afya na zahanati za umma ziko katika mazingira mazuri na zinatoa huduma nzuri kwa wananchi.

Mazingira mazuri hospitalini ni pamoja na kuwepo kwa vitanda vya kutosha kwa wagonjwa, madawa ya kutosha na ya viwango bora, vifaa kwa ajili ya kupima na kubaini magonjwa na vifaa na vyumba maalum vya kusaidia watu wanaofanyiwa upasuaji wasipoteze maisha.

Lakini hali ya hosipitali zetu za umma ni hairidhishi. Kwa mfano hospitali ya taifa ya Rufaa Muhimbili ni hospitali madaktari wanalalamika kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawafanya madaktari kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuokoa maisha ya wagonjwa.

Kwa mfano hospitali hiyo ina mashine ya MRI ya kupima na kutambua ugonjwa mbali mbali kwenye mwili ikiwa ni pamoja na kwenye ubongo, uti wa mgongo na kifua.

Lakini cha kushangaza mashine hiyo iliyonunuliwa kwa shilingi zisizopungua Bilioni mbili miaka michache iliyopita, inapungukiwa kifaa cha bei ndogo tu cha kuwezesha watoto kupimwa.

Hivyo watoto wenye matatizo yanayohitaji kupimwa kwa mashine hiyo wanalazimika kupelekwa India au Afrika ya Kusini kwa wale wenye uwezo wa kujigharamia vinginevyo kwa maskini walio wengi huishia watoto wenye matatizo makubwa yanayoitaji utambuzi wa mashine hiyo, huishia kufa.

Aidha madaktari wanalalamika jinsi wanavyoshindwa kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na tatizo la koromeo la chakula kuungana na koromeo la hewa. Mabingwa wa upasuaji wa watoto katika hospitali hiyo wanasema kwa upande wao wanajitahidi kuwafanyia watoto hao upasuaji, lakini watoto hao huishia hufariki dunia kutokana na hospitali hiyo ya Rufaa kukosa vifaa maalum vya kuhudumia watoto hao na vyumba maalumu vya kuwaweka baada ya kufanyiwa operasheni.

“Kinauma sana na kinakatisha tamaa sana kuona kwamba mtoto anafanyiwa upasuaji vizuri lakini anapoteza maisha siku chache baadaye kutokana na kukosekana kwa vifaa na mazingira ya kumwezesha kupona baada ya upasuaji”, anasema Dakta Catherine Mungo’ngo, Bingwa wa upasuaji wa watoto Hospitali ya Rufaa ya Taifa.

Kwa mujibu wa bingwa huyo kwa mwaka huu pekee watoto watatu waliozaliwa na tatizo la la koromeo la chakula kuungana na koromeo la hewa ambao walifanyiwa upasuaji Muhimbili, baadaye walikufa hospitalini hapo kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuwasaidia kupumulia na chumba maalumu cha kuwafanyia uangalizi baada ya upasuaji.

Aidha anasema watoto kati ya 6 hadi 8 wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kwa siku, upasuaji huo huahirishwa kutokana na ukosefu wa vifaa , dawa na chumba maalum cha kuwatunzia baada ya upasuaji.

Ni mtu gani mwenye akili timamu ambaye atafurahia kuona kazi anayoifanya haitoi matunda yanayotarajiwa.? Ni Daktari gani atakayeendelea kufurajhia kazi yake wakati lengo lake la kuokoa maisha ya watu linakwamishwa na mambo yanayowezekana kurekebishwa?

Daktari furaha yake ni kutibu mgonjwa na kuona anapona. Lakini Daktari katika hospitali za serikali atafanyaje kazi yake kuepusha vifo visivyo vya lazima kama hana vifaa vya kufanyia kazi ?

Nionavyo mimi, serikali yetu inapaswa kutafakari tena kwa utulivu na busara kubwa na kuweka mikakati ya kupata suluhisho la kudumu la mgogoro wake na madaktari.

Vinginevyo hata kama wataagizwa madaktari kutoka Ulaya, na wa hapa nchini kufukuzwa kazi au hata kama viongozi wao ‘watashughulikiwa’, tatizo la mazingira ya kazi hospitalini ambalo ni moja ya mambo ya msingi linalosababisha mgomo wa madaktari litakuwa halijashughulikiwa na litaendelea kujirudia hata kama litapoozwa kwa mbinu yoyote ile.

Na ikumbukwe watakaoendelea kuumia zaidi hapa ni wananchi wengi ambao maisha yao yanategemea uwajibikaji wa serikali yao.
Nijuavyo mimi, serikali ya wananchi, madaktari wakiwa ni sehemu ya wananchi, husikiliza kero za wananchi na kuzishughulikia badala ya kutumia mabavu na vitisho. Mungu ibariki Tanzania.
Ananilea Nkya
Executive Director
Tanzania Media Women's Association (TAMWA)
P. O. Box 8981, Sinza-Mori
Dar es Salaam, TANZANIA
Tel: +255-22 2772681 Fax +255 22 2772681 E-mail:ananilea_nkya@yahoo.com
Cellphone:+255-754-464-368

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII