HABARI MPYA LEO  

ICC yatoa hati ya kukamatwa Laurent Gbagbo

By Unknown - Jun 16, 2012

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imetoa hati ya kukamtwa kwa rais wa Ivory Coast aliyetolewa madarakani Laurent Gbagbo, mawakili wake wamesema. Bw Gbagbo amekuwa kwenye kifungo cha nyumbani tangu Aprili kufuatia ghasia zilizodumu kwa miezi minne dhidi ya rais Alassane Ouattara.

Bw Gbagbo alikataa kukubali kushindwa baada ya uchaguzi wa Novemba 2010. Takriban watu 3,000 walifariki dunia katika ghasia hizo. Ameshtakiwa kwa uporaji, ujambazi kwa kutumia silaha na ubadhirifu. Anaweza kutolewa Ivory Coast kwenda kukabiliana na kesi yake huko the Hague katika saa chache zijazo, wakili wake mmoja aliliambia shirika la habari la AFP.

Bw Gbagbo, ambaye alikuwa madarakani kwa miaka 10, anashikiliwa kwenye mji wa Korhogo kaskazini mwa nchi hiyo. Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Luis Moreno-Ocampo alitembelea Ivory Coast katikati ya mwezi Oktoba kufanya uchunguzi juu ya ghasia za baada ya uchaguzi wa nchi hiyo. Alikutana na walioathirika pamoja na serikali na wawakilishi wa upinzani.

Wakati wa ziara yake hiyo, Bw Moreno-Ocampo aliahidi uchunguzi "utakuwa wa haki" na kusema ataweka nguvu zaidi kwa watu watatu hadi sita waliohusika zaidi kwenye mgogoro wa baada ya uchaguzi.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII