HABARI MPYA LEO  

WAVULANA WAONGOZA KIDATO CHA SITA

By Maganga Media - May 2, 2012

Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa Joyce Ndalichako akitangaza matokeo ya kidato cha sita jijini Dar es Salaam




 

BARAZA la Mtihani la Tanzania (Necta), limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita iliyofanyika Februari mwaka huu yakionyesha kuongezeka kidogo kwa kiwango cha ufaulu kwa ujumla huku wavulana waliofaulu wakiwaacha mbali wasichana.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, kati ya watahiniwa 46,499 waliofanya mtihani huo,  wavulana waliofaulu ni 30,466 wakati wasichana ni 16,033. Hata hivyo, kumekuwa na mchuano mkali katika ufaulu kwa asilimia ambao wasichana walipata 87.37 na wavulana 87.69.

Sekondari ya Wasichana ya Marian, Bagamoyo ndiyo iliyoongoza kitaifa na mwanafunzi wake, Faith Assenga ndiye aliyeshika namba moja katika masomo ya Sayansi.

“Katika masomo ya Biashara, aliyeshika nafasi ya kwanza ni Alex Isdor wa Sekondari ya Kibaha na Lugha ni Faridi Abdallah wa Sekondari ya Mpwapwa,” alisema Dk Ndalichako.

Dk Ndalichako alisema kiwango cha kufaulu kwa watahiniwa 46,499; wakiwemo wale wa kujitegemea, kimeongezeka kutoka asilimia 87.24 mwaka jana hadi 87.58 mwaka huu.

Hata hivyo, alisema mwaka huu watahiniwa wa shule wameanguka katika masomo ya kemia, hisabati ya msingi, uchumi na maarifa ikilinganishwa na mwaka jana.

“Masomo ambayo wanafunzi walifanya vizuri zaidi ni Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Fizikia, Elimu ya Mimea, Biashara, Uhasibu na Hisabati daraja la juu," alisema.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII