HABARI MPYA LEO  

Madaraka Nyerere amjibu Mkapa

By Maganga Media - Mar 15, 2012

Rais mstaafu Benjamin Mkapa
ASEMA VINCENT NI MDOGO WAO, ATAKA TUHUMA ZINGINE AJIBU MWENYEWE
Waandishi wetu, Dar, Arumeru 
MADARAKA Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ameibuka na kuthibitisha kuwa Mbunge wa sasa wa Musoma mjini (Chadema), Vincent Nyerere ni mdogo wao na mwanafamilia hiyo, kwani ni mtoto wa baba yao mdogo, Josephat Kiboko Nyerere.

Kauli ya Madaraka imekuja siku chache baada ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa, kudai kwamba hamtambui mbunge huyo kuwa ni miongoni mwa familia ya Mwalimu Nyerere kwani katika kipindi chote alichofanya kazi na Mwalimu, hakusikia jina hilo.

Jumatatu ya wiki, akizindua kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Mkapa aliuambia umati uliohudhuria kwamba hakuwahi kusikia kama kulikuwa na mtoto wa familia hiyo aliyekuwa akiitwa Vincent Nyerere.

Kauli hiyo ilipingwa vikali juzi na Vincent akisema si jambo la ajabu Mkapa kutomfahamu yeye kwasababu Mkapa si sehemu ya ukoo wao huku akimrushia kombora kwamba akiwa madarakani alishinikiza Mwalimu Nyerere kupelekwa Hospitali ya St Thomas, Uingereza, kinyume na matakwa ya familia yao na wakati huo huo, daktari wake Profesa David Mwakyusa alijua maradhi ya mwasisi huyo wa taifa.


Vincent alikwenda mbali zaidi na kumshambulia Mkapa kwa kuongoza ubinafsishaji holela enzi za utawala wake huku akimtuhumu kuuza viwanda na rasilimali za nchi kwa kisingizio cha ubinafasishaji.      

Jana gazeti hili liliwasiliana na Madaraka kutaka kupata ukweli wa kauli hiyo ya Mkapa. Katika jibu lake fupi, Madaraka alithibitisha kuwa Vincent ambaye sasa ni Meneja Mwenza wa Chadema katika kampeni za Arumeru Mashariki, ni mmoja wanafamilia ya Mwalimu Nyerere  ambayo chimbuko lao ni Kijiji cha Butiama mkoani Mara.
Katika jibu lake alilolituma kwa barua pepe Madaraka alisema; “Naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu yanayozungumzwa kwenye kampeni za uchaguzi wa Arumeru; Ili kuepuka kujiingiza kwenye masuala ya kampeni, nitajibu sehemu ndogo sana ya maswali yako”.
Aliongeza “Nataka kuthibitisha tu kuwa Mhe. Vincent Nyerere ni ndugu yetu, mtoto wa marehemu baba yetu mdogo, Mzee Josephat Kiboko Nyerere. Hayo maswali mengine naomba yaelekezwe kwa Mhe. Benjamin Mkapa au Mhe.Vincent Nyerere”.

Maswali mengine ambayo Madaraka aliulizwa na Mwananchi ni pamoja na kwamba; Nani alishinikiza Mwalimu Nyerere kupelekwa St Thomas, Uingereza na kama familia hiyo iliridhia apelekwe Uingereza au nchi nyingine za Kijamaa.

Madaraka pia aliulizwa anamtambuaje Vincent Nyerere, Ni mmoja wa familia hiyo ama la?

Akizindua kampeni za CCM kwenye uwanja wa michezo wa Ngaresero, Usa River Jumatatu wiki hii, Mkapa alisema: 
“Nimefanya kazi na Mwalimu kwa miaka 25, nikiwa mwandishi wake, Waziri na katika muda huo, nimemzika yeye, kaka yake na mama yake mzazi, sijawahi kusikia jina la mtu kama huyo katika familia ya hiyo”.
Vicent alimtaka pia Mkapa kuacha kujiingiza katika masuala ya familia yasiyomuhusu na kwamba akiwa Rais mstaafu, ana kashfa nyingi zinazougusa utawala wake wa awamu ya tatu.



Chadema wazidi kumlipua 

Katika hatua nyingine, Mkapa amezidi kulipuliwa katika kampeni za uchaguzi huo mdogo baada ya mbunge mwingine wa Chadema, Israel Natse wa jimbo la Karatu na Peter Msigwa wa Jimbo la Iringa, kumtaka Rais huyo mstaafu na Serikali ya CCM kumuogopa Mungu kutokana na kuwadanganya wananchi wa Meru kuwa wakimchagua mgombea wa CCM watarudishiwa ardhi yao ambayo inamilikiwa na walowezi.

Wakizungumza katika mikutano tofauti ya kampeni jana, katika Kijiji cha Njeku na Sura, wachungaji hao, walisema kama Mkapa alikaa madarakani miaka 10 akashindwa kurejesha ardhi inayomilikiwa na walowezi itakuwaje, leo yupo nje amshauri Rais Kikwete kurejesha ardhi hiyo?"

Natse alisema, “Ndugu zangu msidanyanyike na kuendelea kuwasikiliza CCM miaka yote wameshindwa kurejesha ardhi ya Meru sasa wanaibuka…..huyo Mkapa alishindwa akiwa rais sasa amekaa nyumbani akisubiri posho ataweza kumshauri rais awarudishie ardhi yetu?” 


Wakati akizindua kampeni za CCM Machi 12 mwaka huu, Mkapa alisema CCM inatambua tatizo kubwa la ardhi katika jimbo hilo kwani kuna ardhi kubwa ambayo inamilikiwa walowezi na kuna maeneo ambayo hayatumiki ipasavyo kwa mujibu wa hati
miliki na tayari utambuzi umefanyika.

Mkapa alisema atamshauri Rais Kikwete kuchukuwa hatua kuhusiana na tatizo hilo, na kama kuna watendaji ambao watakwamisha watachukuliwa hatua.

Naye Mchungaji Msigwa, alisema moja ya sifa ya kuwa  mwana CCM ni kutomuogopa Mungu kwa kuwa mwongo, mtu wa kujipendekeza na mpenda rushwa  mambo ambayo
Chadema hayapo.” 

Alisema tatizo la Ardhi Meru litamalizwa na Wameru wenyewe na sio CCM kwani ndio waliosaidia kutoa ardhi kwa walowezi.
  
CCM wajibu mapigo
Katika kampeni zilizoanza rasmi jana baada ya uzinduzi uliofanyika Jumatatu wiki hii, CCM kimebeba ajenda ya kufuta kile kinachodaiwa kuwa ni uongozi wa kifalme unaotaka kujengwa ndani ya chama hicho.
Ajenda hiyo inatokana na madai ambayo yamekuwa yakitolewa kwenye mikutano ya Chadema kwamba wasimchague mgombea wa CCM, Siyoi Sumari kwani kwa kufanya hivyo watauegeuza ubunge wa Arumeru Mashariki kuwa Ufalme kwani watakuwa wanamrithisha mgombea huyo nafasi iliyoachwa wazi na baba yake mzazi.
Meneja wa kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba akimnadi Sioi jana alisema: “Chadema ndio vinara wa sera ya utawala wa kifalme na kwamba kudhihirisha hilo, baadhi ya wabunge wa chama hicho wameamua kusaidia watoto wao, wake pamoja mashemeji zao kupata nafasi ndani ya Bunge”.
Akihutubia mikutano ya kampeni katika sehemu za Shambarai, Msitu wa Mbogo na Mbuguni madukani, Nchemba aliwashutumu Chadema kwamba ndani ya chama hicho wamekuwa wakipeana nafasi kindugu.
Mwigulu alidai kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho,Dk  Willibrod Slaa baada ya kuacha ubunge aliyekuwa mke wake, Rose Kamili amechaguliwa kuwa mbunge wa Viti maalumu kutoka mkoa wa Manyara.
Kwa upande wake mbunge wa Mtera (CCM), mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde amekipiga vijembe Chadema kwa madai kwamba kinatumia alama ya vidole viwili kama manati huku akiwaambia wakazi wa Shambarai manati kamwe haiwezi kuua tembo.
Lusinde alisema kwakuwa Chadema wamekuwa wakiendeleza sera za matusi katika mikutano yao ya kampeni, nao (CCM) watamwomba mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kuwapa ruksa ya kujibu mapigo.
Naye mbunge wa Simanjiro (CCM) mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka akimpigia debe Sumari alisema atahakikisha anashirikiana naye pindi atakapopatiwa ridhaa kuwa mbunge kutatua tatizo la ajira wilayani humo kwa kuwatafutia ajira katika mgodi wa madini wa Tanzanite One uliopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
  
Wagombea wa pande hizo mbili Sioi wa CCM na yule wa Chadema, Joshua Nassari waliendelea kunadi sera za vyama vyao pamoja na kutoa ahadi kadhaa kwa wapigakura, huku suala la ardhi likionekana kupewa nafasi kubwa katika kampeni hizo.
Sioi kwa upande wake alisema ikiwa atachaguliwa atashughulikia kero za maji, barabara, uhaba wa masoko, ajira na migogoro ya ardhi.
Alisema migogoro ya ardhi wilayani humo ni tatizo la muda mrefu na kwamba suala hilo ni moja ya mambo ambayo atalitafutia suluhu ikiwa atachaguliwa kuwa mbunge.
Alitaja tatizo jingine kuwa ni uhaba wa ajira kwa vijana na kwamba tatizo hilo atalishughulikia kwa kufungua vituo vya elimu ya ujasiriamali wilayani humo ili waweze kutambua njia za kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali.
Naye mjane wa mpigania ardhi ya Wameru,  Nderetwa Kirilo (85), amembariki Mgombea Ubunge  wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Joshua Nassari kwa kumshika kichwa Kaman ishara ya kumkubali na kumtaka kulinda haki  za Wameru kama alivyokuwa mume wake Japhet Kirilo aliyefariki dunia Mei 30 mwaka 1997.

Akizungumza jana nyumbani kwake katika kata ya Poli, mara baada ya kumbariki mgombea ubunge huyo wa  Chadema, alisema yeye anambariki hata kama ni mgombea wa upinzani, ili mradi anaamini kuwa ataleta maendeleo kwa watu wa Meru.


Kwa upande wake Nassari alimshukuru bibi huyo na kumwaahidi kuendeleza aliyoasisi Mzee Kirilo  kwa kutete haki za wameru hasa kaika suala la ardhi.

Naye Nyerere alisema chama hicho, kina ushahidi wa kutosha juu ya utata wa Uraia wa Sumari na kuna taarifa kuwa sio mtoto wa kuzaa wa mke wa Sumari ambaye alikuwa Mtanzania.
“Sisi tunataka sheria ifuate mkondo sio kutaka kusafishana na tunaomba ieleweke kuwa hatumuogopi Siyoi kwani tunajua tutashinda mapema asubuhi”alisema Nyerere.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari juzi,Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi, alisema majibu ya rufani ya Tume ya Taifa ya uchaguzi yatatolewa ndani ya siku saba .
Imeandikwa na Ramadhan Semtawa Dar, Musa Juma, Arumeru
 Source: Mwananchi la leo

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII