Mwalimu mkuu apigwa vibao mbele ya wanafunzi
By Maganga Media - Mar 15, 2012
Raia mmoja wa Uholanzi, Marise Koch, amemfanyia kitendo cha udhalilishaji Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera iliyopo kata ya Rhotia Wilayani Karatu mkoani Arusha kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi na walimu wenzake.
Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa Idara ya Elimu Wilaya ya Karatu na Jeshi la Polisi, zinasema kutokana na udhalilishaji huo, raia huyo wa Uholanzi ameshafunguliwa jalada lenye namba KRT/RB/835/2012 katika kituo cha polisi Karatu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera, Emmanuel Ginwe, alisema alipigwa vibao viwili na Koch baada ya kuwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule. Ginwe alisema tukio hilo lililotokea Februari 14, 2012 majira 4:30 asubuhi ambapo Koch ambaye anafadhili shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi, nyumba za walimu na kompyuta ndogo za wanafunzi kufanyia michezo na kujifunzia kuandika alifika shule hapo kutembelea kama kawaida.
Alisema baada ya kufika shuleni hapo, alikuta walimu wakipanga ratiba ya shule na kuanza kuhoji kwanini walimu hawajaingia madarasani kufundisha wanafunzi ambapo alijibiwa kuwa wamepewa maelekezo ya kuandaa ratiba ya shule na baada ya kumaliza kazi hiyo wataingia madarasani kufundisha.
Hata hivyo majibu ya walimu hao hayakumridhisha Koch na kuamua kwenda ofisini kwa Mwalimu Mkuu na kuanza kumfokea kwamba yeye anafadhili vitu vingi, lakini kumbe walimu hawafundishi na kuanza kukusanya kompyuta zake ndogo kwa lengo la kuzichukua. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo hata hivyo alimsihi asichukue kompyuta hizo, lakini alikataa na alipoona anazuiliwa, alipiga vibao mwalimu huyo huku akiendelea kuzikusanya komputa na kumnasa tena vibao tena mwalimu mkuu na kuchukua kompyuta zake 70 kati ya 93 zilizokuwepo na kuondoka zake.
“Nimedhalilishwa sana mbele ya walimu, wanafunzi na mke wangu ambaye ni mwalimu, namshukru Mungu wakati ananipiga vibao japo ni mwanamke sikuweza kujibu mapigo,” alisemwa Ginwe.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Karatu, Peter Simwanza, alisema kitendo hicho ni cha kiudhalilishaji.
http://maganga-resources.blogspot.com
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII