HABARI MPYA LEO  

Arumeru: Ni vita ya wabunge

By Maganga Media - Mar 16, 2012

  Vijembe na tambo vyatamalaki
  Nassari aendelea kuwelewa mikono
Mgombea ubunge Arumeru  (Chadema), Joshua Sumari,

Kampeni za kusaka ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Aprili mosi mwaka huu, sasa zimegupigwa na tambo za wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku vijembe vikitawala.


Timu ya wabunge wa CCM ilikishambulia Chadema kuwa hakina uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wa Arumeru Mashariki kutoakana na kutokuwa na serikali. Wabunge hao Livingstone Lusinde (Mtera), Suleiman Said Jafo, (Kisarawe) na Lekule Laizer (Longido) walitoa shutuma hizo katika mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari, katika Kata ya Mbuguni.

Lusinde aliwaambia wananchi waliohudhuria  mikutano katika vijiji vya Msitu wa Mbogo na  Shambarai kuwa ilani ya maendeleo inayotekelezwa ni ya CCM ambacho ndicho chenye serikali. “Wana-Arumeru mchagueni Sioi ndiye anaweza kusikilizwa na serikali, angalieni sana wanakuja kuwadanganya muichukie CCM, nawashauri mtuchagulie Sioi ndiye anayeweza kusikilizwa na Rais wenu,” alisema Lusinde aka Kibajaj.



Alisema kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki madiwani wote wanatokana na CCM, hivyo  kuchagua mbunge wa chama kingine kutawarudisha nyuma  katika harakati za kutafuta maendeleo. Aliwataka wasikubali kupandikiziwa chuki na hasira na kumnyima mgombea wa CCM kura kwani hiyo ni mbinu chafu inayotumiwa na Chadema kujinufaisha kisiasa.

“Tunajua wanapita kueneza chuki dhidi ya CCM, lakini najua wana-Arumeru Mashariki hamtakubali kurubuniwa na kukubali kumpigia kura mgombea tofauti na CCM, naomba muwashauri na wale ambao hawapo katika hadhara hii,” alisema Lusinde. Kwa upande wake, Jafo aliiponda Chadema kwa kueneza propaganda za upotoshaji ukweli wa mambo hasa kwa kueneza kuwa CCM ni cha wazee, madai aliyosema si ya kweli. “Hawa watu hawana sera, hebu angalia wabunge waliopo hapa yupi mzee nawashauri muwapuuze, CCM imejaa vijana simnatuoana hapa,” alisema na kuongeza: “Hawa wamekosa hoja, sasa wanapandikiza chuki, CCM ndicho kinaweza kuwatoa hatua moja kwenda mbele katika maendeleo.”

Naye Laizer aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutorudia makosa waliyofanya mwaka 1995 ya kuchagua mbunge wa upinzani. “Naamini bado hamjasahau kosa mlilowahi kufanya la kuchagua Mbunge wa upinzania. Je, mlipomchagua mlimwoana hapa?” alihoji na kuongeza: “Sasa nawasihi mpeni kura zenu Sioi.”
Alisema  kuwa  amekuwa mbunge kwa kipindi kirefu na kwamba wabunge wa upinzani hawahudhurii vikao vya maendeleo katika ngazi ya mkoa. “Mfano ni kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), hawahudhurii na mfano ninaowapa ni Jimbo la Arusha, Mbunge wa jimbo hilo hajawahi kuhudhuria kikao hicho toka achaguliwe, hawana nia ya dhati hawa,” alisisitiza Laizer.

Akijinadi, Sioi Sumari aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumchagua ili ashirikiane nao kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili. “Nimepita hapa wakati wa kura za maoni, tumezungumza nanyi, lakini sasa ninaomba mnipe kura ili tupambane pamoja kutatua kero mlizonazo zile zitakazokuwa juu ya uwezo wetu nitazipeleka mbele,” alisema.

MJANE WA KIRILO AMBARIKI NASSARI
Wakati wabunge wa CCM wakisaka kura kwa Sioi, jana mjane wa mtetezi wa haki za Wameru kabla ya Uhuru wa Tanganyika, kutoka Meru, Japhet  Kirilo, amembariki mgombea wa Chadema, Joshua Nassari kwa kumshika kichwani na kumtaka kutetea na kulinda haki za Wameru kama alivyofanya mumewe. Mjane huyo, Nderetwa Kirilo (85), kizungumza nyumbani kwake katika Kata ya Poli, baada ya kumbariki Nassari, alisema kuwa alimpa baraka hizo bila kujali anatoka chama gani, bali anaamini kuwa ataleta maendeleo kwa watu wa Meru.

“Mimi mume wangu aliyezaliwa mwaka 1921 Mzee Kirilo alishirikiana na Nyerere na wakati mwingine kulala hapa kwangu, wakiwa katika harakati za kudai uhuru wa Taifa letu na pia Wameru walichangisha fedha walizoweka ndani ya chungu maalum na kumwezesha mume wangu aliyeacha kazi ya udaktari na kwenda Umoja wa Mataifa kudai haki ya ardhi ya Wameru,” alisema Mama Kirilo.

Alisema kuwa mumewe alikuwa mwanaharakati wa siasa ambaye alithubutu kuacha taaluma yake na kuingia katika ulingo wa siasa kwa kutetea watu wa Meru, ambao walimchangia kwa moyo mmoja na kupata nauli ya kwenda Umoja wa Mataifa kudai ardhi ya Wameru. “Sasa niliposikia huyu kijanja wetu amejitokeza katika siasa na kugombea nafasi hii ya kutuwakilisha, mimi nambariki Mungu amtangulie ili akienda bungeni aweze kuwa chachu kwa kutetea ardhi ya Wameru,” alisema Kirilo.

Nassari alimshukuru bibi huyo na kumuahidi kuendeleza aliyoasisi Mzee Kirilo, aliyefariki dunia mwaka 1997 kwa kutetea haki za Wameru hasa ardhi. “Bibi mimi sitakuwa msaliti, naomba unitetee na kuniombea kwa Mungu ili anibariki nitakapopata ubunge,” alisema Nassari.

FEDHA ZA TASAF
Akiomba kura katika Kata ya Songoro kwenye kijiji cha Sura na kijiji cha Ndatu, Nassari alisema kuwa endapo atachaguliwa atawatetea bungeni wananchi wa eneo hilo kuhakikisha fedha zilizoliwa na wajanja za Mfumo wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Sh. million 26 za ujenzi wa barabara ya  Nkoakirika hadi kijiji cha Sura zilizotolewa mwaka jana zinapatikana na kufanya kazi iliyokusudiwa. Nassari alisema kuwa kijijini hapo kuna mradi wa maji toka mwaka 1992 ambao hata hivyo, hadi leo haujatekelezwa na hakuna maelezo yoyote yanayotolewa, hivyo aliomba kupewa ridhaa ya kuwa mbunge ili akawatoe panya katika halmashauri ya Arumeru wanaotafuna fedha za umma.

Meneja wa Kampeni, Vincent Nyerere, alisema anaishangaa serikali kwa kupeleka magari ya programu za maji kwa kila wilaya na mikoa, lakini hakuna maji yanayopelekwa kwa wananchi na kuahidi kuwa ikiwa Chadema kitashinda na kushika dola, watauza magari yote ili kupeleka maji kwa wananchi. Nyerere ambaye ni Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), alitahadharisha Polisi kuwa makini na kikosi cha vijana wa CCM kutoka Musoma na basi maalum kwa lengo la kuleta vurugu kwenye kampeni hizo, na kwamba wao hawahitaji vurugu kwa kuwa ushindi upo kwao.

Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, aliwaomba wananchi hao kuzingatia maadili ya kabila lao kwa kuchagua mbunge anayeyafuata. Mchungaji Natse alisema kuwa anaishangaa serikali kusisitiza sera ya Kilimo Kwanza wakati utekelezaji wake ni hafifu na kuwapelekea wakulima pembejeo za kilimo wakati msimu wa kilimo ukiwa umepita.

SOURCE: NIPASHE
http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII