HABARI MPYA LEO  

Watumieni viongozi wa dini kuwasaidia matatizo yenu

By Maganga Media - Feb 28, 2012

Usichoke!      Timiza malengo yako!!

KARIBU shule zetu zote zina utaratibu wa kuwa na vipindi vya dini.

 Kwa shule za kutwa mara nyingi vipindi hivi hufanyika mara moja ama mbili kwa wiki.

Kwa shule za bweni, mara nyingi kila siku hasa jioni na asubuhi wana muda maalumu kwa ajili ya vipindi vya dini.

Pia wanafunzi hawa wa  bweni wana bahati nyingine ya kuwa na siku moja katika juma ambayo   mara nyingi huwa Ijumaa, ambapo huwa kuna muda rasmi wa kipindi cha dini kinachoendeshwa na viongozi wa dini kutoka nje ya shule.

Vipindi hivi ni muhimu sana katika kuwajenga wanafunzi kiroho kwa mujibu wa mafundisho ya dini zao.Pia vinaweza kutumiwa kuwa mkombozi mkubwa  hata wa kimwili.


Nasema hivi kwa sababu, hivi karibuni nilifanya ziara huko Lugoba, Wilaya Bagamoyo,  mkoni Pwani.  Nilikutana na wanafunzi  waliokuwa wameumizwa  kiroho na wazazi wao. Hawakujua wamweleze nani awasaidie matatizo yao.

Watoto hawa walikuwa wanateseka baada ya wazazi wao kupokea mahari kutoka kwa wanaume na hivyo kuwalazimisha kulala na wazee hao waliowatolea mahari.

Kutokana na adha waliyokuwa wanaipata mpaka wakati mwingine kulazimika kulala porini, walikuwa hawana imani hata na walimu wao,  kwani jamii ya eneo hilo inaamini kuwa walimu wanajua hali hiyo na wamepewa fedha ili kunyamazia matendo hayo.

Katika hatua kama hii ambapo unafanyiwa unyama na mzazi na hata walimu, kimbilio lako la kwanza ni viongozi wako wa dini.

 Waeleze jinsi hali uliyonayo inavyokuumiza, pia kama unaona hakuna msaada, nenda polisi, kwa viongozi wa serikali ya kata ama hata kwa ofisi za wilaya kueleza tatizo lako.

Kumbuka kuwa, hata kama katika vyombo vyote hivyo kuna watu wasio waadilifu, huwezi kukosa mmoja   atakayekusaidia.

Pia kumbuka kuwa, vyombo vya habari ni moja ya nyenzo muhimu ya kuhakikisha sauti za wanyonge zinasikika.

Hivyo basi, kama katika eneo ulipo unaweza kufikisha kilio chako katika vyombo vya habari, fanya hivyo lengo lako likiwa ni kuhakikisha unapata haki yako ya msingi hasa elimu.

Haitakusaidia kama utataka kujinyonga ama kujidhuru kwa aina yoyote ile, jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa unafanikiwa kukamilisha ndoto yako kwa gharama yoyote ile.

Usikubali mtu yeyote yule akatishe ndoto yako kirahisi, utakavyo shindwa kwa namna yoyote ile utakuwa umemnufaisha yeye.
Naamini kuwa viongozi wa dini ni waadilifu vya kutosha, pia kama huwaamini wanaokuja hapo shuleni, basi tafuta walio juu yao uwaeleze shida yako.

Kwa kufanya hivyo watakusaidia na ndoto yako itafikiwa siku moja.


http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII