Dk Bilal avitaka vyuo vya ufundi kuimarisha mafunzo
By Maganga Media - Feb 29, 2012
MAKAMU wa Rais Dk Mohamed Ghalib Bilal ameitaka Mamlaka ya Mfunzo ya Ufundi Stadi nchini (Veta), kuhakikisha inatoa mafunzo ya Ufundi yatakayowasaidia wanafunzi katika kupambana na ushindani wa soko la ajira la Afrika Mashariki.
Akizindua Chuo cha Veta, wilayani Makete ambacho ujenzi wake umeigharimu Serikali Sh 2.8 bilioni, Dk Bilal alisema hakuna njia ya mkato ya kuweza kuwaandaa Watanzania katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki, zaidi ya kuwapa ujuzi kupitia vyuo vya Veta.
Alisema lazima Veta iwe suluhisho katika kuwaandaa vijana kwenye ushindani wa soko la Afrika Mashariki, vinginevyo Tanzania itaendelea kuwa mahali pa kupokea bidhaa na wataalamu kutoka nchi nyingine za jumuiya hiyo, huku Watanzania wakishindwa kuvuka mipaka.
Alisema Serikali imeamua kujenga chuo hicho, baada ya kubaini kuwa kila wilaya inahitaji kuwa na chuo cha ufunzi kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi au sekondari, na kukosa nafasi za kuendelea na masomo ya juu, kujiunga na mafunzo ya ufundi ili waweze kujitegemea. “Naomba Veta iwe suluhisho la matatizo ya ajira nchini na ufumbuzi juu ya ushindani wa soko la ajira, Afrika Mashariki, kama hatutaweza kuwaandaa vijana wetu, basi tujue hii milango ya soko huria inayofunguliwa itatuumiza,” alisema Dk Bilal.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Makete, Dk Binirith Mahenge alisema ufunguzi wa chuo hicho ni ukombozi kwa wanafunzi wa Makete, ambao wengi wao ni watoto yatima baada ya wazazi kufariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi. “Wale watoto yatima mliokuwa mkiwasikia Makete ndio hawa wamekuwa na wameshahitimu masomo yao, bila hiki chuo tatizo tusingekuwa tumelitatua hivyo tunaishukuru Serikali,” alisema.
Awali, Naibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Phillip Mulugo alisema kila mwaka zaidi ya wanafunzi 1 milioni wanaingia kwenye soko la ajira baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya juu.
http://maganga-resources.blogspot.com
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII