Wanafunzi msipende lifti!
By Maganga Media - Feb 28, 2012
|
YAWEZEKANA ni kwa sababu ya shida ya usafiri, lakini pia hata kupenda vitu vya bure kunaweza kuwa moja ya sababu inayofanya wanafunzi wengi kupenda kusubiri magari ya lifti badala ya kutumia yale ya abiria.
Wakati wale wanaosoma shule za katikati ya mji hupenda kuomba lifti kwenye magari madogo, wale wanaosoma shule za pembezoni, hutegemea lifti za magari makubwa.
Kwa wanafunzi wanaosoma shule za kutwa zilizopo katika maeneo ya Pugu na Chanika, mara nyingi utawakuta wamepanda kwenye magari ya takataka bila hata kujali harufu kali zinazotokana na mabaki ya taka zinazobebwa na magari haya.
Pia wale wa Kongowe, Mji Mwema, Kibada, wanaosoma shule zilizopo kwenye barabara ya New Bagamoyo ama Morogoro wao utawakuta zaidi kwenye malori ya mchanga.
Kwa jumla aina zote hizi za usafiri zina madhara yake, ni wiki iliyopita tu tulisikia wanafunzi walionusurika katika ajali ya gari la taka lililopata ajali huko Pugu.
Ikumbukwe kuwa magari mengi haya ya taka ni mabovu, hivyo kupata ajali ni jambo linalotarajiwa wakati wowote.
Yawezekana katika maeneo haya kuna tatizo kubwa la usafiri, lakini uamuzi wa wanafunzi hawa kuamua kuomba lifti katika malori haya siyo wa kuungwa mkono hata kidogo.
Ni vema wakatafuta njia nyingine ikibidi kushirikisha polisi wa usalama barabarani ili kuhakikisha wanasafiri kwa magari ya abiria ambayo yana bima inayowalinda wasafiri.
Pia hali kadhalika kwa malori ya mchanga, hali ipo hivi hivi. Jambo la msingi ni wanafunzi kutambua kuwa mna haki ya kutumia usafiri rasmi wa abiria, siyo malori.
Kwa upande wa wale mnaotegemea lifti za magari madogo, hatari kubwa inayowakabili ni kubakwa ama kushawishiwa na kujikuta mnaingia kwenye mitego ambayo mwisho wake ni kukatisha masomo yenu.
Pia nimegundua kuwa mpo baadhi ya wanafunzi ambao licha ya kupewa fedha za kutosha na wazazi wenu, mnatumia lifti hizi kama sehemu ya mitego yenu.
Kumbukeni kuwa, jambo la msingi kwenu kwa sasa ni elimu tu, hayo mengine yote mtayakuta, na madhara ya kuyakimbilia kabla ya muda kufika ni makubwa kuliko mnavyo tarajia.
Siku za nyuma kidogo tulisikia baadhi ya watu waliokuwa wanawapa watu lifti na katika hayo magari wanapuliziwa madawa, unakuja kujikuta umefikishwa mahali usipopajua.
Nadhani utashukuru angalau utakapojikuta umefikishwa huko, lakini ukiwa hai kuliko ufike huko ukiwa maiti.
Maisha yako yana thamani kuliko kitu chochote kile, hakikisha unayalinda kwa gharama yoyote ile, usikubali kuyachezea hata kidogo.
Dunia ya sasa imebadilika sana, siyo ya kumwamini kila unayemuona. Hata katika haya malori mnaweza kujikuta mnabakwa mkiwa humohumo ndani ya hayo magari.
Sasa kwa nini uhatarishe maisha yako? Yalinde kwa gharama yoyote, magari ya abiria yapo kwa ajili yetu wote. Hakikisha unayatumia kadri iwezekanavyo, hizi lifti za watu msiowajua zitawaponza.
|
from: http://www.mwananchi.co.tz/magazines/33-maarifa/20637-madhara-ya-lifti-ni-makubwa-kwa-wanafunzi.html
http://maganga-resources.blogspot.com
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII