HABARI MPYA LEO  

Umbali mrefu kwenda shule unavyowakwaza wanafunzi wa kike Kilosa

By Maganga Media - Feb 28, 2012


 


WAHENGA walithamini mno elimu na ndio maana walitunga misemo mbalimbali kuhusu umuhimu wake.
Baadhi ya misemo hii ni: Elimu ni bahari, haina moswisho; Elimu ni maendeleo na elimu ndiyo msingi wa maisha.

 Kimsingi,  misemo yote hii inajaribu kuonyesha ni jinsi gani sekta ya  elimu ilivyo muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Hata hivyo, baadhi ya jamii nchini mpaka sasa hazijatambua umuhimu wa elimu hasa kwa watoto wa kike. Imani kubwa iliyopo katika jamii hizi ni kwamba hapaswi kusoma kwa kuwa ni mtu wa kuolewa na kuzaa.

Pia wako wanaokwenda mbali na kuamini kuwa mtoto wa kike hana akili za kusoma,hivyo kumsomesha ni kupoteza muda na rasilimali za wazazi ama walezi.

Kwa upande mwingine, baadhi ya maeneo nchini, wazazi na walezi wametambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.

Hata wazazi maskini wanajihimu kusomesha watoto wao wakiamini katika ule msemo wa wahenga kuwa elimu ndiyo msingi wa maisha.

Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo haya, ikiwamo wilaya ya Kilosa, iliyopo mkoani Morogoro, wanafunzi hawa wa kike wamekuwa wakikumbana na changamoto kedekede ambazo zimekuwa zikiwakwaza katika safari yao ya kuisaka elimu.

Kutokana na changamoto hizi zikiwamo kubwa za umbali wa maeneo zilipo shule, ukosefu wa mabweni na matukio ya mimba, baadhi ya wasichana wamekuwa wakikatisha masomo, jambo linalotia doa azma ya Serikali kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya elimu.

Grace Nzongo  ni mwanafunzi wa kidato cha pili  katika Shule ya Sekondari Chanzuru wiilayani humo   anayesema japo anapenda kusoma, lakini baadhi ya mambo yanamkwaza katika maisha yake ya kila siku.

Kwa mfano, anasema analazimika kutembea umbali wa kilomita 30 kila siku kwenda shule, jambo analosema linamchosha kiasi cha kushindwa kuzingatia taaluma.

“Natembea kilometa 30 kila siku kwa maana ya kwenda kilometa 15 na kurudi kilometa 15. Kwa hiyo nalazmika kuamka asubuhi saa kumi na moja na ninafika shuleni saa tatu.

Huwa nakuta kipindi   cha kwanza kimeisha, inaniumiza sana lakini nitafanyaje na mimi nataka kusoma?”anasema.

Grace anaeleza kuwa wazazi wake ni wakulima masikini ambao wameshindwa japo kumnunulia baiskeli inayoweza kumsaidia kumfikisha shule na kurudi nyumbani kwa haraka.

Shule anayosema nayo haina mabweni ambayo labda yangeweza kuwasitiri wanafunzi wa aina ya Grace.Uongozi wa shule unasema wazazi hawana mwamko wa kujenga mabweni hayo, licha ya kamati ya shule kuwahi kupendekeza suala hilo.

Kwa Grace kutembea umbali huo mrefu tena pekea yake, kunamweka katika wakati mgumu kwa kuwa mara kwa mara anakumbana na vishawishi vya wanaume waendesha pikipiki wanaotaka wampe lifti.

Lakini wapo hata wanaofikia kumrubuni kwa kutaka kumpa pesa za matumizi.

 “Shule kuwa mbali ni kikwazo, wakati mwingine nakuwa nimechoka nakutana na mwendesha bodaboda ananiambia njoo nikupe lifti, nikikataa ananitishia ntakupiga au ntakufanyia kitu kibaya.

 Kwa hiyo najikuta nakubali, lakini wakati mwingine nakuwa nimeshachoka najikuta nakubali. Sasa yote hayo ni changamoto,”anaeleza masaibu anayokumbana nayo na kuongeza:
“Ni muhimu hosteli zikawepo shuleni ili nitumie muda wangu mzuri kusoma na kufaulu, pia itanisaidia kuepukana  na vishawishi, maana   katika familia tupo sita, lakini niliyebahatika kufaulu na kwenda shule ni mimi peke yangu.”

Ndoto ya Grace ni kuja kuwa daktari na ndiyo maana anasema pamoja na vikwazo anavyopata, bado anasoma kwa bidii ili afaulu masomo ya sayansi.

Mkuu wa shule hiyo, Raphael Mpalala anakiri kuwa umbali mrefu ni tatizo siyo tu shuleni kwake, lakini katika wilaya nzima ya Kilosa.
Ni kwa sababu hiyo anasema wanafunzi wengi wamekuwa wakiacha shule, huku wengine wakipata ujauzito.

Anatoa mfano wa mwaka 2010/2011 ambapo wanafunzi sita wa kike waliacha shule kutokana na shule hiyo kuwa mbali na makazi yao.

“Yapo mambo mengi ambayo ni changamoto kwa wanafunzi wa kike. Kwa  mfano,  hapa  shuleni hatuna huduma ya chakula, walimu shule nzima tuko watatu.

Wanafunzi nao wanatembea umbali mrefu, sasa ukiyachanganya yote haya unakuta mwanafunzi hana hamu ya kusoma, jambo ambalo pia linachangia wanafunzi wengi kufeli katika mitihani yao ya mwisho,’’anabainisha mwalimu huyo.

Akizungumzia namna ya kutatuta changamoto hii na nyinginezo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, anasema mkakati wa mkoa ukiondoa ujenzi wa mabweni, ni pamoja na kuhakikisha kila kata inakuwa na sekondari, huku kila wilaya ikiwa ni sekondari ya kidato cha tano na sita.

Anaamini ikiwa kila kata itakuwa na shule yake, itasaidia wanafunzi kutotembea umbali mrefu na hivyo kusaidia kupunguza idadi ya wanafunzi wanaofanya vibaya katika mitihani yao.

Mpango mwingine anaosema ni  kuanzisha  mfuko wa elimu  katika kila wilaya ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali  zinazoikabili sekta ya elimu katika mkoa huo.

“Nimepania lazima heshima ya elimu katika mkoa huu ipande kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anayefikia umri wa kwenda shule anakwenda, kila kata iwe na sekondari na kila tarafa iwe na kidato cha tano na sita.  Kwa kuwa naamini elimu ni sekta mama, sekta mtambuka na maendeleo yoyote ili yapatikane, lazima elimu iwepo,”anasema Bendera
Kwa upande wake, Ofisa Taaluma Sekondari wa Wilaya ya Kilosa, Jaka Omari, anasema ukitoa umbali mrefu,lipo suala la wanafunzi kutokuwa na elimu ya kujitambua, hivyo baadhi kujikuta wakiingia kwa wepesi katika vishawishi viovu.

“Naamini wakiwepo walimu wa kutosha wa elimu ya kujitambua, itawasaidia wanafunzi kujitambua na hivyo kujiepusha na vishawishi ambavyo mwishowe  vinawaharibia masomo na maisha kwa jumla,”anasema.

KILOSA ina ukubwa wa kilometa 14,245,kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 ina jumla ya wakazi  4,191,000 huku makadirio kwa mwaka 2011 ya idadi ya watu ikiwa ni 5,087967.

Kilosa ina tarafa tisa ambazo ni Mikumi, Gairo, Ulaya, Masanza, Kimamba, Nongwe, Kidete, Magole na Kilosa, huku ikiwa na vijiji 164, vitongoji 1010 na kata 46.
From: http://www.mwananchi.co.tz/magazines/33-maarifa/20640-umbali-mrefu-kwenda-shule-unavyowakwaza-wanafunzi-wa-kike-kilosa.html
http://maganga-resources.blogspot.com

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII