maonyesho kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari.
By Maganga Media - Feb 28, 2012
|
NI jambo lililo wazi kwamba hamasa ya wanafunzi wa Kitanzania kusoma masomo ya sayansi iko chini. Kushuka kwa hamasa hiyo kunachangiwa na mambo mengi ikiwamo kutokuwepo kwa msukumo wa kutosha wa kuyaendeleza masomo hay. Kwa nchi kama Uganda, wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kusoma sayansi ni jambo la kawaida, jambo ambalo linaweza kufanyika hata hapa nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi nchini, Shirikisho la Wanasayansi Chipukizi Tanzania(YST) linatarajia kuandaa maonyesho kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari. Mwenyekiti wa YST, Gothbert Kamugisha anasema wanafunzi hao watapata fursa ya kuonyesha kazi za tafiti za kisayansi watakazozifanya ikiwa ni njia ya kuwahamasisha kupenda masomo hayo.
Anasema kuwa maonyesho hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho hilo yatafanyika Oktoba 24 na 25 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Anasema kuwa tafiti hizo zitahusu masuala ya mienendo ya watu na sayansi ya jamii, Kemia, Fizikia, Sayansi ya Hesabu, teknolojia, Biolojia na Sayansi ya Ekologia na kwamba majaji katika onyesho hilo watatoka katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
“Shule ambazo zitapenda kushiriki zitapewa semina elekezi kuhusu namna ya kufanya ugunduzi na tafiti mbali mbali. Semina hizi tayari zimeanza kufanyika katika baadhi ya mikoa,” anasema Kamugisha na kuongeza:
“Zawadi za washindi tumezigawa katika makundi. Kundi la kwanza itakuwa ni tafiti za wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne na kundi la pili ni kuanzia kidato cha tano na cha sita. Watakaoibuka washindi watapewa kikombe na fedha.”
Anaeleza kuwa mbali na zawadi hizo kwa wanafunzi, shule 100 ambazo mapendekezo ya tafiti zitakazofanywa na wanafunzi wake yatapita, zitawezeshwa vifaa vya kuwawezesha wanafunzi hao kufanya tafiti zao. Katika mpango huo anasema kuwa wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya kisayansi nje ya madarasa ya kawaida, jambo ambalo litawafanya waweze kufahamu vizuri manufaa ya sayansi katika maisha yao.
Anasema wanafunzi hao wataamua wenyewe vitu wanavyotaka kukifanyia utafiti kulingana na mazingira wanayoishi na kwamba YST itawaelekeza namna ya kuboresha tafiti zao. Anasisitiza kuwa shule zote zitakazoshiriki maonyesho hayo zitapewa usafiri wa kuja kwenye maonyesho ikiwa ni pamoja na malazi kipindi cha maonyesho.
“Juhudi zimeanza kufanyika ili kuwaunganisha wanafunzi watakaofanya tafiti hizi na vyuo vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya tafiti na sekta binafsi ili kuweza kupata ushauri kuhusu namna ya kufanya tafiti mbalimbali” anasema.
Kutekeleza mpango huu, YST inashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia ili kuyafanya maonyesho hayo kuwa na mwamko mkubwa. “Wanafunzi watakaoshiriki maonyesho haya pia watapata umahiri wa kutafiti na kushughulikia matatizo mbalimbali katika jamii watakazokuwa wakiishi na pia itawasaidia kujiajiri jambo ambalo litawainua kiuchumi” anasema Kamugisha
Akizungumzia malengo, Kamugisha anasema maonyesho hayo yataongeza ari ya wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na kufanya tafiti za kisayansi katika shule za sekondari na vyuo vikuu.“Hii itakuwa ni kiunganishi kati ya shule za sekondari na vyuo vikuu na kuufanya umma kupenda masuala ya sayansi na teknolojia,” anasema.
Mkurugenzi wa Habari na Nyaraka wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH), Dk Raphael Mmasi anasema washindi katika utafiti huo watawawezeshwa kwa kupatiwa vifaa vya kufanyia utafiti ili waweze kujiajiri wenyewe. “Lengo letu ni kuwapatia vifaa vya kufanyia utafiti kwa kuwa wakijiajiri wenyewe, watajenga ajira kwa wenzao. Tafiti nzuri ni manufaa kwa Taifa” anasema Dk Mmasi.
Anasema kuwa somo la sayansi linatakiwa kujengewa misingi ya kupendwa na wanafunzi tangu shule ya msingi na kwamba COSTECH inaiunga mkono YST na kuwatambua wanafunzi wote ambao tafiti zao zitakuwa bora.Anasisitiza kuwa kazi ya tume hiyo ni kuhamasisha na kuamsha mwamko wa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi…. “Lengo ni kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma sayansi. Kwa mfano, mwaka jana tuliwafadhili wanafunzi 295 kusoma vyuo vikuu mbalimbali, lengo ni wao kumaliza na kuwafundisha wengine.” |
http://maganga-resources.blogspot.com
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII