Wanazuoni wahofia ajira!
By Maganga Media - May 3, 2012
Baadhi ya wasomi mbalimbali wamekuwa katika hali ya sintofahamu baada ya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa siku ya wafanyakazi duniani iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Tanga. Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii, utata huo ulikuja baada ya Rais kusisitiza juu ya elimu ya ujasiliamali na kujiajiri ikiwa ni njia ya kutatua tatizo la ajira.
"Tumeelekeza kuwa mitaala ya shule na vyuo izingatie kutoa elimu na mafunzo yanayotakiwa na soko la ajira. Kadhalika vijana wapate elimu na mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri. Kwa ajili hiyo tumesisitiza somo la ujasiriamali kufundishwa shuleni na vyuoni."
Rais alitolea mfano juu ya wanaosoma masomo ya lugha kama Kiswahili na Kiingereza kuwa njia muafaka kwao ni kujiajiri. Ni kweli kuwa huu ni muda muafaka wa kutathimni juu ya mitaala yetu na namna tunavyolitazama soko la ajira. Ni vyema vijana wakaandaliwa kuwa na ujuzi binafsi utakao wasaidia wao wenyewe kuwa tayari kujiendesha kimaisha. Tuachane na kauli kuwa kuwa msomi ni lazima uajiriwe serikalini. Tuachane na mtazamo wa White Color Jobs.
Soma hotuba kamili juu ya kipengele hicho cha ajira kama kilivyokuwa.
Ukosefu wa Ajira
Ndugu wafanyakazi;
Nchi yetu, kama zilivyo nchi nyingi duniani inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira hasa kwa vijana. Ukosefu wa ajira hapa nchini umefikia karibu asilimia 12 kwa mujibu wa sensa ya kazi ya mwaka 2006. Taarifa ya Utafiti ya Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) inaonyesha kuwa mnamo mwaka 2011 watu wapatao milioni 200 hawakuwa na ajira duniani, na inategemewa kwamba idadi hiyo itaongezeka na kufikia watu milioni 204 mwaka huu (2012) na ifikapo mwaka 2013, idadi hiyo itafikia watu milioni 209.
Kwa kutambua umuhimu wa kuchukua hatua thabiti za kukuza ajira ili kupunguza tatizo hilo, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2005 ya CCM iliipa Serikali yake lengo la kuzalisha ajira milioni moja. Bahati nzuri lengo hilo liliweza kufikiwa na kuvukwa. Ajira milioni 1.2 zilizalishwa. Katika kipindi hiki Serikali imejipanga kuzalisha ajira maradufu ya zile za kipindi cha kwanza.
Kwa ajili hiyo hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa ili kuzalisha ajira mpya nyingi zaidi. Niruhusuni nitaje baadhi tu ya hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa:
1. Tumefanya maboresho katika kuendeleza rasilimali watu hasa katika nyanja za elimu, mafunzo na ujuzi ili kuwawezesha wahitimu wake wawe na sifa za kuajiriwa ndani na nje ya nchi na uwezo wa kujiajiri wenyewe. Tumeelekeza kuwa mitaala ya shule na vyuo izingatie kutoa elimu na mafunzo yanayotakiwa na soko la ajira. Kadhalika vijana wapate elimu na mafunzo yatakayowawezesha kujiajiri. Kwa ajili hiyo tumesisitiza somo la ujasiriamali kufundishwa shuleni na vyuoni. Hii itawawezesha vijana kujua namna ya kuanzisha na kuendesha shughuli za uzalishaji na huduma zitakazowapatia mapato.
2. Tumeanza kuchukua hatua za kutekeleza mkakati maalum wa kuwatafutia Watanzania ajira nchi za nje. Hatua hizo zimewezesha vijana wa Kitanzania 1,327 kupata ajira katika nchi za Oman, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Wizara ya Kazi na Ajira katika mwaka 2011/12. Lengo letu ni kuona vijana wengi zaidi wanapata ajira katika nchi hizo na nyinginezo nyingi duniani kama walivyo majirani zetu.
3. Kwa nia ya kuwasaidia vijana kupata ajira hapa nchini, tumeamua kuunda Kamati Maalum za kukuza ajira katika kila Wizara na Mikoa. Kwa kuanzia Wizara sita na Halmashauri 12 katika mikoa ya Lindi na Mtwara zimeunda Kamati Maalum na madawati ya kukuza ajira. Wizara hizo ni pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi pamoja na TAMISEMI.
4. Tumeendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo wa Tanzania kushiriki katika maonyesho ya kila mwaka ya nguvu kazi/jua kali ya nchi za Afrika Mashariki. Lengo letu kuu ni kuwapatia wajasiriamali wetu wadogo (ambao ndio wengi) fursa ya kujifunza, kupata soko na kutumia fursa hizo kukuza shughuli zao wazifanyazo. Kwa kufanya hivyo, Watanzania watanufika na fursa za itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki. Wastani wa wajasiriamali 106 wamekuwa wakiwezeshwa kushiriki maonesho husika (Nguvu Kazi/Jua kali) kila mwaka kwa kipindi cha miaka 13 sasa.
5. Kupitia mradi wa kujenga usawa wa jinsia na ajira bora kwa wanawake, hadi kufikia mwezi April 2012 kiasi cha shilingi bilioni 1.23 kimekopeshwa kwa wanawake. Wanawake wapatao 4,097 wamenufaika kupitia SACCOS za wanawake katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke na Tukuyu. Baada ya mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya hizo, tunajipanga kueneza mpango huu nchi nzima.
6. Mtakumbuka kuwa mwaka 2006 tulianzisha Mfuko wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo. Tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila mikoa ya Tanzania Bara na shilingi milioni 200 kwa Mjini Magharibi na shilingi milioni 100 kwa mikoa mingine minne ya Unguja na Pemba. Kwa upande wa Tanzania Bara, hadi kufikia mwezi Desemba, 2010, ilitolewa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 47.3 kwa wajasiriamali 73,496, SACCOS 192 na vikundi vya kiuchumi 86. Wote hao wamejiajiri na kuwawezesha watu kadhaa kupata ajira. Tumekamilisha tathmini ya mpango huu na makakati unaandaliwa wa kuuendeleza. Shabaha yetu ni kuongeza fedha na kuboresha mfumo wa ukopeshaji, utafutaji na usimamizi wa wakopaji.
7. Serikali imeendelea kuwekeza katika shughuli za ujenzi wa majengo na miundombinu, shughuli ambazo zimekuwa zikitoa ajira nyingi kwa wananchi. Katika miaka ya 2009, 2010 na 2011 peke yake shughuli hizi zimepanuka sana. Jumla ya miradi mikubwa 8,870 yenye thamani ya shilingi trilioni 7.6 ilisajiliwa na Bodi ya Wakandarasi. Miradi hii imezalisha ajira 59,743 kati ya mwaka 2010 na 2012 kwa wahandisi na wataalamu wa fani mbali mbali, mafundi, vibarua, wenye magari ya uchukuzi, madereva na waendesha mitambo, mama lishe, wauzaji wa vifaa vya ujenzi, na watoa huduma za ujenzi.
Uwekezaji uliofanywa katika sekta ya ujenzi sio tu umeongeza ajira bali pia umeongeza mzunguko wa fedha nchini. Umesaidia kupunguza umaskini. Tutaendelea kuwekeza zaidi katika sekta hii ya ujenzi na sekta nyinginezo zenye kuzalisha ajira kwa wingi.
8. Tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo Serikali ilikuwa mwajiri mkubwa siku hizi ni sekta binafsi. Ni kwa sababu hiyo basi, Serikali inahimiza kukuza uwekezaji kutoka ndani na nje, na kuendeleza sekta binafsi ya wazawa nchini. Tumeendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Viwanda hususan kwenye Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZ) na Maeneo Maalum ya Mauzo Nje (EPZ). Mwaka wa jana peke yake, jumla ya miradi mipya 17 yenye thamani ya dola za Kimarekani 112 ilipatikana na kutoa ajira 8,059 kwa wananchi. Matarajio yetu kwa mwaka huu ni kupata miradi mipya 23 itakayozalisha ajira 14,500.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII