Tanzania yaunga mkono Sahara Magharibi iwe huru
By Maganga Media - May 10, 2012
Bernard Membe (Mb) akizungumza na wanhabari jijini Dar es Salaam
TANZANIA haijabadili msimamo wake katika kuwaunga mkono watu wa Sahara Magharibi kuhusu haki yao ya kujitawala kutoka mikononi mwa Morocco. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema pia Tanzania imeisihi Morocco irudi kuwa mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ili kuwa na mazungumzo ya pamoja baina yao, wananchi wa Sahara Magharibi na Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu mgogoro huo.
Kuhusu tatizo la kumpata Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Membe alisema Tanzania inaungana na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kumuunga mkono mgombea kutoka Afrika Kusini kwenye nafasi hiyo, Nkosazana Dlamini-Zuma dhidi ya mgombea anayetetea uenyekiti huo, Jean Ping.
Nchi Wanachama wa AU zinatarajiwa kupiga kura na kumchagua Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo Julai mwaka huu wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi mjini Lilongwe, nchini Malawi.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII