HABARI MPYA LEO  

SIMBA, TP MAZEMBE na APR kuisaidia familia ya Mafisango.

By Maganga Media - May 28, 2012


KLABU ya soka ya Simba kwa kushirikiana na klabu za Tp Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na APR ya Rwanda, zipo katika mchakato wa kuandaa mechi maalum kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa mchezaji wao, Patrick Mutesa Mafisango.
 
Mafisango ambaye alifariki dunia wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari alizikwa nyumbani kwao Kinshasa, Congo.
 
Makamu Mwenyekiti wa Simba Geofrey Nyange 'Kaburu' amesema jana kwamba, hawana budi kumuenzi mchezaji huyo kutokana na kutoa mchango mkubwa kwa timu hizo enzi za uhai wake.
 
Aliongeza kuwa fedha zitakazopatikana zitapelekwa katika familia ya Mafisango ili ziweze kusaidia wake na watoto wake. Aidha, Simba imezishukuru timu za Yanga kupitia wazee wa baraza, Azam Fc, Coastal Union, Villa Squad , kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom na Kampuni ya bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro kwa michango yao ya hali na mali baada ya kutokea kwa msiba huo.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII