HABARI MPYA LEO  

Nassari ajutia kauli yake.

By Maganga Media - May 11, 2012

MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ameelezea kusikitishwa na tafsiri potofu kuhusu kauli yake ya kuhimiza Serikali kutekeleza wajibu na majukumu yake kwa umma, ikiwamo kutafutia ufumbuzi suala la tatizo la ardhi linaloikabili jimbo lake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Nassari ambaye tayari amehojiwa kuhusu kauli zake alizotoa kwenye mkutano wa hadhara alisema kauli yake ililenga kuisukuma Serikali kutatua kero za wananchi na kamwe haikulenga kugawa nchi wala kumzuia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kufika Arusha kama inavyotafsiriwa.

Mbunge huyo ambaye jalada la mahojiano na maelezo yake kwa  polisi limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa uamuzi wa hatua zaidi ya kisheria alisema hata alipohimiza uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Kata ya USA-River alilenga kuwaeleza  polisi hali halisi ya jinsi wapiga kura wake wanavyojisikia kwa uchunguzi kuchukua muda mrefu.

Alisema hofu kuhusu uchunguzi wa tukio hilo inatokana na mazingira ya kifo hicho, hali ya kisiasa jimboni humo baada ya uchaguzi mdogo na joto lililopanda kuhusiana na matukio ya uvamizi wa mashamba na kusisitiza kuwa kamwe hakulenga kuchochea vurugu au kumzuia Rais kutekeleza wajibu wake kama inavyotasiriwa na baadhi ya watu.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII