HABARI MPYA LEO  

MAHAKAMA YAKATAA OMBI LA LULU

By Maganga Media - May 8, 2012

Lulu (katikati) akiingia mahakamani na askari magereza wa kike.
Hapa ni karibu na mlango wa kuingia katika chumba cha mahakama.

 

Msanii wa filamu za maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, jana alipandishwa tena kizimbani mara ya tatu katika kesi ya mauaji ya Kanumba inayomkabili ambapo mawakili wanaomtetea wakiongozwa na Kennedy Fungamtama waliwasilisha ombi la kurekebisha umri wa mshitakiwa huyo kuwa miaka 17 na si 18 kama ilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda aliomba wapewe muda zaidi kwa sababu bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo. “Kesi hii imekuja mahakamani hapa kama ya mauaji na upelelezi bado haujakamilika. Tunaposema haujakamilika, tunapeleleza kila kitu, likiwamo suala la umri,” alieleza Kaganda. Alisema hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa kilichowasilishwa mahakamani hapo, linasomeka Diana Elizabeth wakati mshtakiwa ametajwa mahakamani hapo, kwa jina la Elizabeth Michael. “Tunaomba muda tuweze kuchunguza kuhusu umri wa mshtakiwa kwa sababu aliwaeleza polisi kwamba ana umri wa miaka 18 halafu mawakili wake wanakuja kueleza hapa mahakamani kwamba ana umri wa miaka 17,” alidai Kaganda. Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa kutokana na mvuto wa kesi hiyo katika jamii, wanaomba wapewe muda zaidi kufanya upelelezi ili kumtendea haki mshtakiwa huyo.

 Kuhusu cheti hicho kusomeka Diana Elizabeth, Wakili Fungamtama alikiri na kudai kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa Wakristo kuwa na majina mawili. Fungamtama alidai kuwa hawana pingamizi na maombi ya upande wa mashtaka kwamba wapewe muda zaidi wa kufuatilia cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa, ingawa alidai kuwa suala hilo halina ugumu. Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi Augustina Mbando alisema: “Mahakama imesikiliza maombi yaliyoletwa na Fungamtama na Kaganda na imeona kesi iliyopo hapa ni ya mauaji na jinsi kesi hii ilivyo, hatuwezi kufanya hoja yoyote hadi upelelezi utakapokamilika.”

“Kama defence (upande wa utetezi) wana maombi yoyote wanaweza kufanya hivyo kupitia Mahakama Kuu,”

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21, mwaka huu itakapotajwa tena. Inadaiwa kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam msanii huyo wa kike, alimuua Kanumba. Jana Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 2:50 asubuhi akiwa peke yake kwenye gari linalobeba mahabusu, huku akisindikizwa na magari mengine mawili. 





Chanzo - http://www.globalpublishers.info

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII