Traore Rais wa Mpito Mali
By Maganga Media - Apr 13, 2012
| Traore baada ya kuapishwa Bamako |
Dioncounda Traore ameapishwa kuwa Rais wa mpito wa Mali kuashiria kurejea kwa utawala wa kiraia baada ya mapinduzi kutokea mwezi uliopita nchini humo. Serikali ya spika huyo wa zamani sasa ina siku 40 za kuandaa uchaguzi.
Waandishi wanasema muda huo huenda usitoshe kuandaa uchaguzi hasa kwa kuzingatia eneo la kaskazini kuwa mikononi mwa waasi. Majukumu ya kiongozi wa mapinduzi Kepteni Amadou Sanogo hayajajulikana.
Bw Traore aliapishwa na Rais wa mahakama Kuu Nouhoum Tapily katika hafla fupi mjini Bamako.
Mataifa ya Afrika Magharibi yaliondoa vikwazo vyake kwa Mali baada ya Kepten Sanogo kukubali kuachia madaraka. Kabla ya makubaliano yaliyofikiwa Ijumaa aliomba Jumuiya ya Ecowas kusadia kuwaondoa waasi wa Tuareg na wenzao wapiganaji wa Kiislam ambao wameliteka miji muhimu ya kaskazini.
Hata hivyo hata awali alishasema kuwa anachohitaji ni msaada wa vifaa na uratibu akipinga vikosi vya wanajeshi 3000 wa Ecowas kuingilia kati. Pamoja na hayo Ecowas bado inatafakari uwezekano wa kupeleka vikosi na mawaziri wa mambo ya nje wanakutana Alhamis katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan kwa majadiliano.
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII