HABARI MPYA LEO  

Barca Vs Chelsea nusu fainali

By Maganga Media - Apr 5, 2012

Meneja wa muda wa Chelsea Roberto di Matteo amesisitiza watakuwa na mpango madhubuti wa kuifunga Barcelona katika mchezo wa nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya.

Roberto Di Matteo meneja wa muda wa Chelsea
Roberto Di Matteo (Chelsea)
Barcelona itakabiliana na Chelsea ili kutafuta nafasi ya kucheza fainali mwezi wa Mei mjini Munich baada ya Chelsea kuitoa Benfica kwa jumla ya mabao 3-1 kwa ushindi wa mabao 2-1 kwenye pambano la robo fainali uwanja wa Stamford Bridge siku ya Jumatano.

Nae meneja wa muda wa Chelsea Di Matteo anasisitiza Chelsea haiogopi mtazamo wa kukabiliana na mabingwa watetezi wa Ulaya ambao pia wanapewa nafasi kubwa ya kunyakua tena ubingwa huo na kurudiwa kilichotokea katika uwanja wa Stamford Bridge mwaka 2009 wakati wa nusu fainali ambapo bao la dakika za mwisho lililokuwa na utata la Andres Iniesta lililoivusha Barcelona hadi fainali.

Di Matteo alisema: "Litakuwa jambo la faraja kukabiliana na timu bora duniani katika michezo miwili. Tutatafuta mikakati itakayotumiwa na wachezaji wetu na hatimaye kuwafunga Barcelona." "Itakuwa ni mchanganyiko wa kucheza kwa nguvu zetu zote huku tukitilia maanani ubora wao.

"Bila shaka wana wachezaji wenye vipaji binafsi ambao ni tishio kubwa na ni hatari sana, lakini hatuna budi kucheza mchezo wetu kwa nguvu zetu zote."

KAULI YA MOURINHO
Sambamba na Hilo, Kocha wa Real Madrid ya Uhispania, Jose Mourinho, amesema hatazamii kukutana na klabu yake ya zamani, Chelsea, katika fainali ya klabu bingwa barani Ulaya. Real itakutana na Bayern Munich ya Ujerumani katika nusu fainali, baada ya kuishinda Apoel Nicosia, nayo Chelsea itacheza na Barcelona.
Kocha Josee Mourinho (Real Madrid)

Tarehe 17 Aprili, Bayern Munich itacheza na Real Madrid, na tarehe 18 Aprili, Chelsea itacheza na Barcelona.

Tarehe 24 Aprili, Barcelona itacheza na Chelsea, na 25 Aprili Real Madrid imepangwa kucheza na Bayern Munich.

Lakini Mourinho, ambaye amelalamika kwamba inaelekea maafisa wa soka wanaipendelea Barcelona, amesema hatazamii kukutana na The Blues (jina la utani la Chelsea). "Inaweza kuwa Bayern au Barcelona, lakini sidhani itakuwa ni Real Madrid na Chelsea, na tunajua ni kwa nini", alisema. "Barcelona sio tu wanatazamiwa kufuzu, bali wanatazamiwa sana kufuzu", aliongezea.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII