HABARI MPYA LEO  

RAIS WA MALI APINDULIWA MADARAKANI

By Maganga Media - Mar 22, 2012


  Rais wa Mali aliyepinduliwa leo , Amadou Toumani Toure

Ulianza kama uasi wa kawaida wa wanajeshi wa ngazi za chini, wanaolalamikia kushindwa kwa serikali kuwapa silaha za kutosha kupambana na waasi, lakini umemalizikia kuwa mapinduzi ya kijeshi, baada ya wanajeshi hao kuviteka vituo vya redio na televisheni ikulu ya rais, wakiwa wamepambana na upinzani mdogo sana.

Baada ya masaa kadhaa ya kutokusikikana chochote redioni wala kuonekana kitu kwenye televisheni, tangazo lilipita kwenye televisheni hiyo ya taifa likisomeka: "tangazo kutoka kwa wanajeshi kuja hivi punde", likisindikizwa na picha za vidio za muziki wa rhumba wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi. Hatimaye saa moja na nusu asubuhi kwa saa za Afrika ya Mashariki, kundi dogo la wanajeshi waliovalia sare zao, lilijitokeza kwenye kioo cha televisheni, na mmoja wao, aliyejitambulisha kama Luteni Amadou Konare akasoma tangazo la kumuondoa madarakani Rais Toure na kuisimamisha katiba ya nchi hiyo, pamoja na kuzivunja rasmi taasisi zote za dola.

Tangazo la mapinduzi
"Sisi walinzi wa Jamhuri na watu wake, tumelazimika kuchukuwa madaraka kutoka utawala ulioshindwa wa Amadou Toumani Toure na tutayakabidhi madaraka hayo kwa serikali itakayochaguliwa kidemokrasia." Alisema Luteni Konare. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wanajeshi hao sasa wameunda chombo walichokiita Kamati ya Kitaifa ya Kurudisha Utawala wa Kidemokrasia baada ya kuwatia nguvuni mawaziri kadhaa wa serikali ya Rais Toure. 

Mwanajeshi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, miongoni mwa walio chini ya ulinzi ni waziri wa mambo ya nje, Soumeylou Boubeye Maiga, na waziri wa mambo ya ndani, Kafouhouna Kone.

Chanzo huru cha habari kimesema kwamba Rais Toure mwenyewe, ambaye mwanzoni walikuwa amezingirwa ndani ya kasri yake, alifanikiwa kuondoka eneo hilo salama. Bado haijulikani alipo rais huyo, ambaye mwenyewe aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1991.
Mapema nyakati za alfajiri kwa saa za Afrika ya Magharibi, milio ya silaha nzito na bunduki ilisikikana karibu na kasri hiyo na katika mji mkuu, Bamako, lakini mapambano hayo hayakuchukuwa muda mrefu wala hakujapatikana ripoti za maafa yake hadi sasa.

Sababu kuu ya wanajeshi hao kuasi na hatimaye kuchukuwa madaraka ya nchi, ni kile walichokiona kama ulegevu wa serikali katika suala la vita dhidi ya waasi wa Toureg, kaskazini mwa nchi hiyo. Kwa kipindi sasa, wanajeshi walikuwa wakilalamikia upungufu wa vifaa vinavyotolewa na serikali kupambana na waasi hao, ambapo mapigano makali katika miezi ya hivi karibuni yamegharimu maisha ya watu kadhaa na kuwalazimisha takribani raia 200,000 kuzikimbia nyumba zao.

Mwezi uliopita mamia ya watu waliandamana katika mji mkuu, Bamako, kuilalamikia serikali kushindwa kuwadhibiti waasi wa Toureg, ambao wengi wao wana silaha kutoka serikali ya zamani ya Libya, chini ya Marehemu Muammar Gaddafi.

CHANZO: DW
Maganga Media

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII