HABARI MPYA LEO  

AJIRA KWA VIJANA SIYO BOMU, Serikali

By Maganga Media - Mar 22, 2012

Waziri wa ajira na Kazi Gaudensia Kabaka
SERIKALI imetoa takwimu za ajira kwa vijana nchini  ikiwa ni majibu kwa kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa ambaye amekuwa akisema tatizo hilo ni kubwa akililinganisha na bomu linalosubiri kulipuka. Lowassa amenukuliwa katika matukio manne tofauti kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mwaka huu, akionya tatizo hilo la ajira kwa vijana kwamba linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Jana, Waziri wa Kazi na Ajira alisema tatizo hilo haliwezi kufafanishwa na bomu na kusema wanaosambaza uvumi huo hawaitendei haki Serikali, kwani tatizo hilo limepungua kutoka asilimia 12.9 mwaka 2000/1 hadi asilimia 11.7, mwaka 2006.

Maana ya ajira
Akinuuku tafsiri inayotumika duniani na kutambuliwa na Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO), Waziri Kabaka alisema maana ya ajira ni shughuli yoyote halali anayoifanya mtu mwenye umri wa kufanya kazi kwa kujipatia kipato na kwa kawaida shughuli hiyo ni ya hiari inayotambuliwa kisheria na hufanywa kwa saa 40 hadi 45 kwa wiki.

Alisema ukosefu wa ajira ni hali ambayo hutokea wakati watu walioko kwenye umri wa kufanya kazi na ambao wangependa kufanya kazi wanatafuta bila ya kuipata.

“Tafisiri hii ya kimataifa haiwajumuishi wale wasiotafuta kazi, wasiopenda kufanya kazi hata kama hawana kazi,” alisema Kabaka na kuongeza:
“Lakini tafisiri inayotumika zaidi Tanzania inatambua wote wasio na kazi na ambao wako tayari kufanya kazi  bila kujali wanatafuta kazi au la na inawahusisha hata  wasio na uhakika wa kufanya kazi hata ya siku moja.”
Alitaja aina tatu za ajira ambazo ni kazi ya staha, kazi chini ya kiwango na ajira maskini.

Alisema ajira za staha ni zile ambazo zina tija kiusalama, heshima haki za wafanyakazi na kipato cha kutosha, wakati ya ile ya chini ya kiwango ni ile ambayo haitoshelezi kutumia uwezo, muda na taaluma yote ambayo ambayo mhusika anayo. Ajira maskini ni ile ambayo kipato kinachopatikana ni cha chini ya kiwango kisichomwezesha mtu kuishi.

Akirejea utafiti wa ILO wa mwaka 2010/11, Waziri Kabaka alisema ripoti hiyo inaonyesha hali ya umaskini na ukosefu wa ajira duniani ni kubwa. Watu 205 milioni dunia kote mwaka 2010 hawakuwa na ajira.
Alisema idadi hiyo ilikuwa sawa na ongezeko la nguvu kazi isiyo na ajira duniani ya watu 27.7 milioni kulinganisha na ile ya mwaka 2007.

Alisema sababu za ongezeko la ukosefu wa ajira kwa mujibu wa ripoti hiyo, ni kutokana na utandawazi, maendeleo ya mawasiliano, mabadiliko ya teknolojia ambayo hayahitaji nguvu kazi nyingi katika utendaji kazi na kudidimia kwa nguvu za kiuchumi hasa katika nchi zinazoendelea.

CHANZO: Mwananchi

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII