HABARI MPYA LEO  

Wazanzibari waliokimbia machafuko mwaka 2001 warejea nchini!

By Unknown - Jul 7, 2012

WAZANZIBARI 38 waliokuwa wakiishi kama wakimbizi katika kambi ya Dadab, Kenya wamerejea nyumbani jana kwa ndege maalumu za Umoja wa Mataifa (UN).

Wazanzibari hao ni sehemu ya raia wa visiwa hivyo walikimbia baada ya machafuko ya kisiasa ya Januari 26 na 27, 2001 ambayo yalisababisha pia vifo vya zaidi ya watu 20, huku wengine wakikimbilia Shimoni, Mombasa.

Jana, ikiwa ni zaidi ya muongo mmoja tangu kuondoka nchini, Wazanzibari hao walirejea kwa ndege za UN, chini ya usimamizi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la umoja huo (UNHCR).

Katika safari hiyo ya kurejea nyumbani, Wazanzibari hao mbali ya kuongozana na maofisa wa UNHCR, pia walikuwamo baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege Zanzibar, baadhi yao walisema wanajisikia furaha kurudi nyumbani ambako sasa kuna amani kubwa kutokana na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mmoja wa wakimbizi hao, Rashid Abdallah Said alisema ameishi kwa muda wa miaka 12 kama mkimbizi nje ya Zanzibar na kwamba maisha yake huko yalikuwa magumu lakini alilazimika kukubaliana na hali hiyo kutokana na kile alichoamini kuwa Zanzibar hakuna amani.

“Tumerejea nyumbani baada kuonyeshwa kanda za Zanzibar ambazo zinaonyesha hali ya amani iliyopo na sisi kwa hiari yetu, tukaamua kurudi bila ya kusukumwa,” alisema Said.

Alisema yeye na wenzake, wanayo furaha kurejea nyumbani Zanzibar kwani hata hali ya mazingira imebadilika... “Tunajisikia furaha sana.”

Kwa upande wake, Mohammed Adama Suleiman ambaye ni mkazi wa Ziwani, Pemba ambaye alikuwa akiishi Somalia alisema waliondoka kwa matatizo ya kisiasa ambayo yalisababisha kukosekana kwa amani...“Sasa Nchi yetu ina amani kwa nini tukae nchi isiyokuwa na amani?”

Suleiman aliwaomba wenzao ambao bado wanaishi kama wakimbizi warejee nyumbani kwani amani tayari imeshamiri.

Mkimbizi mwingine aliyekuwa Somalia, Omari Awesu ambaye ni mkazi wa Jang'ombe, Zanzibar alisema hakuna kitu ambacho kimemrudisha zaidi ya kuchoshwa na maisha Somalia ambayo yametawaliwa na vita... “Wazee wangu pia ni muda wa miaka 12 sijawaona ndicho kitu kikubwa kilichonifanya nirudi nyumbani.”

Awesu alisema hawajashawishiwa na UN kurudi nyumbani bali, waliamua kufanya hivyo baada ya UNHCR kuwashauri kwamba mtu yeyote anayetaka kurudi kwao atasaidiwa.

Ofisa Habari wa UNHCR Austin Makani alisema Wazanzibari hao ambao wamerudi walifanya hivyo kwa hiari yao na hawajalazimishwa.

Alisema UNHCR imewasaidia kiasi cha Dola za Marekani 800 (Sh1.2milioni), kila mmoja kwa lengo la kuweza kujikimu angalau kwa miezi minne.Alisema zaidi ya Wazanzibar 52 bado wako Somalia na hawajataka kurudi wakiwasubiri waliotangulia ili waone maendeleo yao.

“Tutaandaa Filamu maalumu ambazo zinaonyesha hali ya amani ambazo zitawashawishi waliobakia Somali nao waweze kurudi,” alisema Makani.

Wazanzibari hao walikimbia nchini baada ya vurugu za kisiasa zilizotokea baada ya maandamano yalioandaliwa na Chama Cha Wananchi (CUF), mwaka 2001 na kusababisha vifo hivyo.

CUF walikuwa wakipinga ushindi wa matokeo yaliyokipa ushindi CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 wakidai kuwa mgombea wao Maalim Seif Sharrif Hamad ndiye aliyekuwa ameshinda.

Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS

ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII