Baraza la Mawaziri muda wowote
By Maganga Media - May 3, 2012

IKULU imewataka Watanzania watarajie Baraza bora la Mawaziri muda wowote kuanzia leo ambalo limekuwa likisukwa kwa umakini mkubwa na Rais Jakaya Kikwete.Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti la Mwananchi jana kuwa: “Rais anasuka Baraza makini la Mawaziri. Yaani kama ni chakula kikiwekwa mezani kila mtu anatakiwa awe na hamu ya kupakua na kula. Kama ni njaa basi itakwisha nadhani muda si mrefu.” Balozi Sefue alisema jambo zito kama mabadiliko ya mawaziri, linahitaji umakini wa hali ya juu hivyo Watanzania wanapaswa kumpa muda Rais kusuka baraza bora linaloweza kuwa chachu ya ufanisi katika utendaji kazi wa Serikali. “Nadhani, jambo la msingi tumpe muda Mheshimiwa Rais afanye uteuzi wa watu bora. Naamini kiu hiyo itakatwa muda mfupi ujao wala sidhani kama itachukua muda mrefu sana. Watanzania wajiandae kupata baraza bora,” alisema. Balozi Sefue alisema Rais Kikwete anajua Watanzania wana kiu ya kupata Baraza jipya la Mawaziri lakini akasema mkuu wa nchi anachokifanya sasa ni kuhakikisha kiu hiyo inakatwa kwa kuwapa wananchi baraza bora. Alisema haki itatendeka katika suala hilo kwa kuwawajibisha wanaopaswa kuwajibishwa kadri Rais mwenyewe atakavyokuwa amejiridhisha kwa tuhuma zinazowakabili. Aliongeza kwamba Rais atafanya uamuzi huo kwa kuangalia matakwa ya Watanzania na aina ya mawaziri ambao taifa linawahitaji kwa sasa. Balozi Sefue alipoulizwa kwa nini Ikulu haikutoa agizo kwa mawaziri hao kujiuzulu kabla ya Rais kuchukua hatua, alisema uwajibikaji wa namna hiyo ungekuwa ni sawa na kuwalazimisha kitu ambacho siyo kizuri kwani kila mtu alipaswa kujipima mwenyewe. |
Follow Maganga Media on Twitter, Feel free to like and comment Facebook. Stay updated via RSS
ANDIKA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII